
Makamu Mkuu wa Chuo cha Ushirika Moshi (MoCU), Profesa Alfred Sife, amesema kuwa ujenzi wa Kampasi mpya ya Kizumbi (KICoB) mkoani Shinyanga chini ya Mradi wa Elimu ya Juu Kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza Machi 5, 2026 mkoani Kilimanjaro, Prof. Sife ameeleza kuwa ujenzi wa jengo la Kitaaluma umekamilika kwa asilimia 98.3 na tayari umechochea ongezeko la thamani ya ardhi kutoka shilingi milioni 2.6 kwa kiwanja cha mita 20 x 20 mwaka 2022 hadi kufikia shilingi milioni 5.0 Juni 2025 huku kodi za nyumba zikiongezeka kutoka shilingi 50,000 hadi 150,000 kwa mwezi kwa nyumba za vyumba viwili, hali iliyowahamasisha wakazi kuwekeza katika ujenzi wa nyumba na biashara mpya.

Profesa Sife ameongeza kuwa bweni jipya lililokamilika kwa asilimia 99.5 limewezesha chuo kutoa makazi salama kwa wanafunzi 204 na limeongeza mapato ya chuo kwa shilingi milioni 48.96 kupitia ada za malazi na kuzalisha ajira kwa wakazi wa eneo hilo kupitia huduma za ulinzi na usafi, pamoja na kuimaimarisha ustawi wa kijamii kwa wanafunzi, hususan wa kike, kwa kuwapa mazingira salama na rafiki ya kujifunza.

Katika Kampasi Kuu ya Moshi, maboresho ya miundombinu yamehusisha ukarabati wa maabara ya kompyuta pamoja na ujenzi wa jengo la kitaaluma lenye Ofisi, vyumba vya mihadhara na ujenzi wa njia rafiki kwa watu wenye ulemavu. Hatua hii imeboresha mazingira ya kujifunza na kutoa fursa kwa wanafunzi 24 wenye ulemavu kupata upatikanaji bora wa rasilimali za kielimu.

Profesa Sife amesema kuwa maboresho haya yameimarisha ujumuishi na usawa katika elimu ya juu, na kuhakikisha kila mwanafunzi anapata nafasi sawa ya kufikia huduma za chuo.

Profesa Sife amesema kuwa mradi wa HEET umeongeza uwezo wa MoCU kufundisha na kutoa huduma bora, huku ukichangia moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi ya Shinyanga. Alisisitiza kuwa takwimu za ongezeko la thamani ya ardhi, mapato ya chuo, ajira mpya na ujumuishi wa wanafunzi wenye ulemavu zinaonyesha wazi athari chanya za mradi huu kwa chuo na jamii inayozunguka kampasi.


