Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, ambaye pia ni rais wa Chama cha Skauti Tanzania Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa chama hicho kinasaidia kujenga mshikamano wa vijana, kukuza maadili na uzalendo kwa vijana Nchini.



Waziri Mkenda ameeleza hayo Januari 9, 2026 Mkoani Pwani akifungua Mkutano wa 7 wa chama hicho, akisisitiza kuwa, Wizara itaendelea kuimarisha uskauti katika taasisi za elimu ili kiendelee kujenga ustawi wa nchi.



Naye, Mdhamini wa Chama cha Skauti Tanzania, Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga wa Jimbo Katoliki la Mbeya na Rais wa TEC, amewahimiza Maskauri kutambua heshima na thamani wanayopewa na jamii, kuilinda, na kutekeleza majukumu yao kulingana na mahitaji ya taifa na jamii ya Watanzania.



Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa, amesema kuwa katika Karne ya 21 umuhimu wa Skauti umeongezeka maradufu, akieleza kuwa ni nguzo ya ulinzi na usalama wa nchi, uraia mwema na elimu ya kujitegemea.



Wakizungumzia katika mkutano huo, wanachama wa Skauti Mohamed Ramadhani na Mariam Juma wamesema wataendelea kudumisha mshikamano na kuilinda nchi pamoja na jamii kwa ujumla.