
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amesisitiza wajibu wa vyuo vya elimu ya juu na vya kati kuzingatia malengo ya kuanzishwa kwake.

Akizungumza Januari 07, 2026 wakati wa ziara yake katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), amesema kuwa si vyema chuo kutoa kila aina ya programu bila kujiuliza kama zinaakisi dhima yake ya msingi, na akasisitiza umuhimu wa MoCU kuendelea kuendeleza wanataaluma na tafiti zinazolenga moja kwa moja ushirika, biashara, ujasiriamali na maendeleo ya jamii.

Mhe. Ameir amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kujenga taifa lenye rasilimali watu wenye ujuzi na weledi kupitia elimu bora, sayansi, teknolojia na ubunifu.

Alimeipongeza MoCU kwa kuendelea kufanya mapitio ya mitaala na kuandaa mipya inayozingatia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na mahitaji halisi ya sekta ya ushirika na biashara.

Aidha, ameeleza kuwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), Serikali inaliona MoCU kama mdau muhimu wa kimkakati na kwamba ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo makao makuu ya chuo na Kampasi ya Kizumbi mkoani Shinyanga, na akasisitiza ushirikishwaji wa wadau wote muhimu katika mchakato wa mapitio ya mitaala ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri alitoa wito kwa uongozi, wahadhiri na wanafunzi kuendelea kulinda na kuenzi utambulisho wa MoCU kama kitovu cha elimu ya ushirika na biashara. Alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuwezesha vyuo vya elimu ya juu nchini kuboresha sera, miundombinu na rasilimali watu ili kuhakikisha vinazalisha wahitimu wenye maarifa, ujuzi na maadili yanayokidhi mahitaji ya maendeleo ya taifa na kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


