Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, ameielekeza VETA Moshi kuimarisha ushirikiano na makampuni na viwanda ili kuongeza ajira kwa wahitimu na matumizi ya teknolojia mpya, kwa kuzingatia uelekeo wa nchi kama ulivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, sera za kisekta na miongozo mbalimbali ya kitaifa.



Mhe. Ameir ametoa maelekezo hayo Januari 07, 2026, alipotembelea chuo hicho, akisisitiza kuwa ushirikiano huo unaboresha mafunzo na kulingana na mahitaji ya soko la ajira.



Aidha, amesema kuwa utekelezaji wa mafunzo ya sekta ya madini kupitia programu jumuishi ya ufundi wa teknolojia ya uchimbaji madini kwa kushirikiana na Chemba ya Madini Tanzania utawezesha utoaji wa mafunzo yanayoakisi mahitaji halisi ya sekta hiyo muhimu kwa taifa.



Amesema kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika kuongeza fursa na kuinua ubora wa mafunzo ya ufundi stadi kwa kununua vifaa vya kisasa, kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na ujenzi wa vyuo vipya vya VETA 64 nchini.