
Katika kuhakikisha kuwa mafunzo ya darasani yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amekutana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzzane Ndomba, kwa mazungumzo ya kina kuhusu namna ya kuwawezesha vijana wanaohitimu vyuoni kupata mafunzo ya vitendo sehemu za kazi.
Mkutano huo umefanyika Septemba 24, 2025 katika ofisi za ATE jijini Dar es Salaam, ambapo Prof. Nombo alieleza kuwa Serikali imefanya mapitio ya Sera ya Elimu na maboresho ya mitaala katika ngazi zote za elimu ili kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa kazi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Aidha, Prof. Nombo alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa mafunzo kwa walimu walioko kazini ili kuboresha mbinu za ufundishaji, akieleza kuwa ufundishaji bora ndio msingi wa kuwajengea wanafunzi ujuzi wa maisha na ajira.
Akifafanua lengo la ziara hiyo, Prof. Nombo alisema kuwa ni kujadiliana na ATE juu ya njia bora za kuwashirikisha waajiri katika kusaidia vijana waliopo vyuoni au waliomaliza masomo kupata mafunzo ya vitendo sehemu za kazi.
Kwa upande wake, Bi. Suzanne Ndomba-Doran alieleza kuwa ATE imekuwa na utaratibu wa kusaidia wanafunzi kupata mafunzo kwa vitendo kwa kuwapeleka kufanya kazi katika viwanda na makampuni wanachama wa chama hicho. Alitolea mfano wa Mradi wa Kukuza Ujuzi wa Vijana unaotekelezwa na ATE, ambao umewezesha zaidi ya vijana 1,000 waliomaliza kidato cha nne kupata mafunzo ya miezi sita katika vyuo vya ufundi, na baadaye kupelekwa makampuni na taasisi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya vitendo. Baadhi ya vijana hao wamefanikiwa kupata ajira kupitia utaratibu huo.
Bi. Ndomba pia alitoa wito kwa Watanzania kupenda kujifunza kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa gharama nafuu, akisisitiza kuwa ujuzi unaweza kupatikana bila kujali kiwango cha elimu rasmi alichonacho mtu.