Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia TAEC itahakikisha elimu na taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya nguvu za nyuklia ikiwemo mradi wa kimkakati wa uzalishaji umeme wa nyuklia zinapatikana na kutolewa kwa wadau wote.



Hayo yameelezwa na katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo septemba 2025 Viena Austria katika kikao maalum kati ya Tanzania na Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Miundombinu ya Nyuklia wa IAEA, Bi. Liliya Dulinets.



Katika Kikao hicho kilichofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 69 IAEA unaoendelea ameuhakikishia Uongozi wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki (IAEA) kuwa Tanzania imejipanga katika kutoa elimu ili kuhakikisha ushiriki wa wadau katika mradi.



Hatua hii inalenga kuongeza uelewa wa kitaifa na kuwezesha ushiriki wa wadau katika nyanja za elimu, utafiti, teknolojia na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia mradi huu wa kimkakati.

Kwa upande wake Bi. Dullinets aliujulisha Ujumbe wa Tanzania kuwa, IAEA itatoa ushirikiano wa kutosha katika ujenzi wa miundombinu ya nyuklia. Aidha, alishauri kuwa taarifa zote muhimu kuhusu utekelezaji wa mradi ziwafikie wadau wote na pia zitumike kuboresha na kuimarisha mpangokazi wa mradi wa nyuklia.

Prof. Nombo, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano Mkuu wa 69 wa IAEA unaojumuisha Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Afya; Wizara ya Nishati pamoja na Wizara ya Nishati, Maji na Madini Zanzibar.