Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) na Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, ameielekeza Menejimenti ya Chuo hicho kusimamia kwa makini wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ili ikamilike kwa wakati na kwa viwango.



Mhe. Pinda ametoa agizo hilo Juni 04, 2025 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa, mabweni, maktaba, jengo la utawala pamoja na miundombinu mingine katika Kampasi Kuu ya Butiama kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi Tanzania (HEET).



Amesisitiza kuwa wananchi wana matarajio makubwa ya kukamilika kwa miradi hiyo kwa ufanisi.



Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha miradi hiyo inanufaisha Chuo, akifafanua kuwa tayari kiasi cha shilingi bilioni 102.5 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi Kuu ya Butiama na Kampasi ya Tabora.



Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Lesakit Mellau, ameeleza kuwa Chuo kimeanza kutoa mafunzo na idadi ya wanafunzi inatarajiwa kufikia 6,000 baada ya kukamilika kwa miundombinu inayoendelea kujengwa.