Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amekutana na Mkurugenzi wa Karibu Tanzania Organization (KTO), Ndugu Maggid Mjengwa, katika ofisi za Wizara jijini Dodoma kwa mazungumzo ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa programu mbalimbali za elimu kupitia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs).



Mazungumzo hayo yaliyofanyika Oktoba 10, 2025 yamelenga kuboresha utekelezaji wa programu zinazotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara na KTO, hususan zile zinazolenga kuwajengea uwezo wananchi kupitia elimu jumuishi na endelevu.



Miongoni mwa programu zilizojadiliwa ni Elimu Haina Mwisho, inayolenga wanawake vijana waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali. Kupitia FDCs, washiriki wa programu hii hupata fursa ya kuendelea na elimu ya sekondari, ufundi stadi na elimu ya amali.



Programu nyingine ni Elimu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECD), pamoja na Mpira Fursa, inayolenga kukuza vipaji na maendeleo ya soka kwa vijana wa kike na wa kiume.



Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Elimu ya Ufundi (TVET), Dkt. Erick Mgaya, ambaye anasimamia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ameshiriki mazungumzo hayo.



Prof. Nombo amepongeza mchango wa KTO kama mdau wa maendeleo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo katika kuendeleza programu za serikali zinazolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa elimu inayojali ujumuishi, stadi za maisha na maendeleo endelevu.