
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kupeleka mbele ajenda ya kuboresha Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Tarehe 21 Januari 2026, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb), akiambatana na Naibu Waziri Mhe. Wanu Hafidh Ameir (Mb), Katibu Mkuu Prof. Carolyne Nombo, Naibu Katibu Mkuu Prof. Daniel Mushi pamoja na viongozi waandamizi wa wizara hiyo, walikutana na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square jijini Dodoma.

Mazungumzo hayo yalijikita katika kutathmini mafanikio yaliyopatikana na changamoto zinazokabili sekta ya elimu, sambamba na kupanga mikakati ya kuongeza uwekezaji ili kupanua fursa na kuboresha ubora wa Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na viongozi wa juu kutoka Wizara ya Fedha akiwemo Naibu Waziri Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) na Kamishna wa Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, pamoja na viongozi wengine waandamizi.


