WADAU WAJADILI MUSTAKABALI WA ELIMU KATIKA MKUTANO WA TATHMINI 2024/25
Wadau mbalimbali katika majadiliano Mkutano wa Mwaka wa Tathimini ya Pamoja ya Sekta ya Elimu 2024/25, Oktoba 23, 2025 Jijini Dodoma.
Wadau mbalimbali katika majadiliano Mkutano wa Mwaka wa Tathimini ya Pamoja ya Sekta ya Elimu 2024/25, Oktoba 23, 2025 Jijini Dodoma.
Mkutano wa Mwaka wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Elimu 2024/25 umeingia katika siku yake ya pili Oktoba 23, 2025 jijini Dodoma, ambapo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewasilisha taarifa ya utekelezaji wa sekta ya elimu kwa mwaka 2024/25.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, ameongoza majadiliano kuhusu taarifa hiyo muhimu, yenye lengo la kuboresha ubora wa elimu nchini na kuhakikisha malengo ya maendeleo ya sekta yanatekelezwa kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Maalum, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Magreth Matonya amesema Serikali inaendesha programu mbalimbali za elimu, ikiwemo ya kubaini wanafunzi wenye mahitaji maalum kuanzia ngazi ya kijiji kwa ajili ya maandalizi ya kujiunga na shule.
Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Fredrick Salukele, amesema kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia katika shule za amali na vyuo vya ufundi nchini.
Mwakilishi wa Ubalozi wa Uingereza, Godfrida Magubo, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu katika ngazi zote za elimu ambayo imechochea ufundishaji na ujifunzaji.
Magubo amesema hayo Oktoba 22, 2025 jijini Dodoma katika Mkutano wa Mwaka wa Tathimini ya Sekta ya Elimu, ambapo amesisitiza matumizi ya teknolojia na takwimu sahihi ili kuwezesha kufuatilia maendeleo ya elimu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali katika kutekeleza Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakidhi mahitaji ya sasa na baadae ya kijamii na kiuchumi.