A. UTANGULIZI
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Programu maalum ya SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED DS/AI+ inayolenga kuongeza na kukuza ujuzi wa vijana wa Kitanzania katika fani za Sayansi ya Takwimu, Akili Unde na Sayansi Shirikishi (Data Science, Artificial Intelligence and Allied Sciences) kulingana na mahitaji ya soko la ajira nchini na kuchangia katika maendeleo ya Taifa, Kikanda na Kimataifa.
Wizara inatangaza fursa za ufadhili wa masomo katika ngazi ya Shahada ya Umahiri kwa wahitimu wenye ufaulu wa juu zaidi kwenye masomo ya Data Science, Artificial Intelligence, and related disciplines kama vile Machine Learning, Cybersecurity, Computer Science, Computer Engineering, and Software Engineering.
B. MAENEO YA UFADHILI
SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED (DS/AI+) itatoa ufadhili kwa ajili ya masomo ya shahada ya umahiri unaojumuisha:
- i. Ada ya Mafunzo;
- ii. Posho ya Chakula na Malazi;
- iii. Posho ya Vitabu na Viandikwa;
- iv. Mahitaji Maalum ya Vitivo;
- v. Utafiti;
- vi. Bima ya Afya.
C. VYUO VIKUU VINAVYOLENGWA
Ufadhili utatolewa kwa waombaji wenye udahili katika Taasisi ya Teknolojia ya India Madras (Indian Institute of Technology Madras - IITM) Kampasi ya Zanzibar.
D. MUDA WA UFADHILI
Wanafunzi watakaofadhiliwa, watagharimiwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Mwaka wa fedha 2026/2027.
E. SIFA ZA WAOMBAJI WA UFADHILI
Ufadhili huu utatolewa kwa wanafunzi waliohitimu shahada ya kwanza wenye sifa zifuatazo:
- i. Awe Mtanzania;
- ii. Awe na udahili wa kusoma Shahada ya Umahiri katika fani ya Sayansi ya Takwimu na Akili Unde (M.Tech. in Data Science & Artificial Intelligence) katika Taasisi ya Teknolojia ya India Madras, Kampasi ya Zanzibar;
- iii. Awe na umri usiozidi miaka 35;
- iv. Awe amefanya tahasusi za sayansi katika Kidato cha Sita na kuwa na ufaulu wa juu, hususani katika somo la Hisabati (Advanced Mathematics);
- v. Awe na GPA isiyopungua 3.8 katika shahada ya kwanza.
NYARAKA ZA KUWASILISHA
- i. Barua ya udahili (Admission letter);
- ii. Nakala ya kitambulisho cha NIDA;
- iii. Cheti cha kuzaliwa;
- iv. Vyeti vya Shule ya Sekondari;
- a. Cheti cha Kidato cha Nne (Form IV);
- b. Cheti cha Kidato cha Sita (Form VI);
- v. Cheti cha Shahada ya Kwanza;
- vi. Academic Transcript ya Shahada ya Kwanza;
- vii. Wasifu wa mwombaji (CV).
G. MASHARTI YA UFADHILI
Mwanafunzi atakayepata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIP EXTENDED (DS/AI+) atatakiwa kuzingatia masharti yafuatayo:
- i. Anapaswa kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili wa Masomo kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;
- ii. Anapaswa kuwa na akaunti ya Benki kwa ajili ya fedha atakazolipwa moja kwa moja;
- iii. Hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila barua ya idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia;
- iv. Hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa na chuo husika;
- v. Ikiwa mnufaika ataghairi fursa ya ufadhili kabla ya kuanza masomo, atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwenda kwa: Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia, S.L.P. 10, 40479 Dodoma. Barua pepe: ps@moe.go.tz
H. UTARATIBU WA KUWASILISHA MAOMBI YA UFADHILI
- i. Maombi ya Ufadhili wa Masomo yawasilishwe kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kiunganishi kifuatacho: temis.moe.go.tz;
- ii. Muombaji anatakiwa aweke mawasiliano yake pamoja na barua pepe na namba ya simu.
I. MUDA WA KUWASILISHA MAOMBI
Maombi ya kuomba Ufadhili wa Masomo yawasilishwe kuanzia Mei 29 hadi June 17, 2026.
Imetolewa na:
Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia, Dodoma. Tarehe 26-05-2026
