Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI wanatekeleza Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP). Lengo kuu la mradi huu ni kuhakikisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia yanaboreshwa katika shule za Sekondari. Mradi unatarajiwa kutekelezwa katika eneo la Elimu ya Sekondari Kidato cha Kwanza hadi cha Sita kwa kipindi cha miaka mitano (5) kuanzia 2020/2021 hadi 2024/2025.

Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari unafadhiliwa na Benki ya Dunia kwa mkopo wa fedha za Kimarekani Dola milioni 500 sawa na fedha za Kitanzania Shilingi Trilioni 1.2. Utaratibu wa utoaji wa fedha utazingatia ufikiwaji wa Viashiria vya Matokeo vilivyokubaliwa (Disbursement Linked Indicators - DLIs) kwa gharama ya Dola za Kimarekani milioni 480 na utaratibu wa kawaida wa kugharamia shughuli za uendeshaji wa mradi na ushauri wa kitaalam (Investment Project Financing - IPF) wenye jumla ya US$ milioni 20. 

MALENGO YA MRADI

Lengo kuu la mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari nchini ni kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za Sekondari. Malengo mahususi ni Pamoja na;-

  • Kuongeza fursa ya upatikanaji wa Elimu ya Sekondari
  • Kuweka mazingira salama ya Elimu kwa wasichana waliopo katika Shule za Sekondari; na
  • Kuhakikisha wanafunzi wote wanaoanza masomo ya sekondari wanamaliza Elimu ya Sekondari.

MAENEO YA UTEKELEZAJI WA MRADI

Shughuli zilizobainishwa kwenye rasimu ya andiko la mradi (Project Appraisal Document - PAD) na andiko la utekelezaji wa mradi (Project Operating Manual) zitatekelezwa katika maeneo manne (4) ambayo ni:

  • Kujenga uwezo wa wanafunzi wote hususani wanafunzi wa kike kupata Elimu ya Sekondari na stadi za Maisha;
  • Kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji na matumizi ya teknolojia ya kidijitali (TEHAMA);
  • Kuongeza upatikanaji wa Elimu ya Sekondari na kupunguza vikwazo kwa mwanafunzi wa kike na,
  • Ufuatiliaji, tathmini na uendeshaji wa mradi.

VIASHIRIA VYA UTEKELEZAJI NA UPIMAJI WA MAFANIKIO YA MRADI

Utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) unasimamiwa na viashiria muhimu vya upimaji 12 ambavyo vitatumika katuika kupima mafaniko katika kutekeleza mradi. Viashiria hivyo bi kama inavyoonekana katika jedwali.

Na.

VIASHIRIA

WIZARA

INAYOTEKELEZA

1

Asilimia ya wanafunzi wasichana wanaojiunga na elimu nje ya mfumo rasmi (AEP) kumaliza elimu ya sekondari Kidato cha Nne,

MoEST

2

Asilimia ya wanafunzi wa kike wanaomaliza elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi kidato cha 4 ambao wanajiunga na kidato cha 5 au vyuo vya serikali vya elimu ya kati,

MoEST & PO-RALG

3

Idadi ya shule za sekondari zinazotekeleza Mpango wa Shule Salama na uzingatiaji wa jinsia kufikia 1,000

MoEST & PO-RALG

4

Idadi ya wanafunzi wa kike wanaosajiliwa kidato cha 5 kwenye shule za sekondari za serikali kufikia 40,000

PO-RALG

5

Kuimarisha mfumo wa taarifa/takwimu ili kupunguza mdondoko wa wanafunzi,

PO-RALG

6

Kuimarika kwa ufundishaji na ujifunzaji darasani kwa kutoa mafunzo kwa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati wapatao 20,000 

MOEST

7

Asilimia 50 ya shule za sekondari za serikali zenye walimu wa sayansi na hisabati waliopangwa/ajiliwa kwa kuzingatia mkakati wa upangaji wa walimu (Teacher Deployment Strategy),

PO- RALG

8

Asilimia 50 ya shule za sekondari za serikali kwenye kila halmashauri zenye vitabu vya masomo ya sayansi na hisabati kwa uwiano wa 1:1 au 1:2,

MoEST

9

Idadi ya shule za sekondari za serikali zinazotumia teknolojia ya ICT katika ufundishaji na ujifunzaji kufikia 1300

MoEST & PO-RALG

10

Tathmini ya taifa ya ufundishaji na ujifunzaji kidato cha 2

MoEST

11

Asilimia 50 ya shule za sekondari za serikali kwenye kila halmashauri zenye vyumba vya madarasa kwa uwiano wa 1:50 na matundu ya vyoo kwa uwiano wa 1:25 kwa wasichana na 1:30 kwa wavulana,

PO-RALG

12

Uzingatiaji wa serikali wa upelekaji wa fedha za utekelezaji wa miradi na Elimu Msingi Bila Malipo.

PO-RALG

   

 

KAZI ZILIZOTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA WA 2022/2023

  1. Shughuli mahsusi zitakazotekelezwa na Mradi

Katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023 kilichoanzia mwezi Julai, 2022 hadi Juni, 2023, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja/ikishirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Mradi wa SEQUIP. Utekelezaji wa shughuli za mradi umezingati maelekezo ya Utekelezaji (POM) ambayo yaliwekwa katika mfumo rahisi wa Mpango kazi wa mwaka (Annual Work Plan).

  1.  Ujenzi wa Miundombinu
  • Umeendelea na ujenzi wa shule mpya 231 za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha nne zenye uwezo wa kuwachukuwa wanafunzi 400 kwa maeneo yenye wanafunzi wengi ambapo kati ya hizo, shule 211 zimepokea wanafunzi. Fedha zimeshatumwa kwa ajili ya ujenzi wa shule za kutwa 212 na nyumba za walimu 212 (2 in1) na ukarabati wa shule kongwe 5.
  • Umeendelea na ujenzi wa shule 26 za Kidato cha 5&6 (A- LEVEL) za kisasa kwa wanafunzi wa kike ili kuongeza nafasi za kujiunga na kidato cha 5&6 na kupunguza changamoto za upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi hao. Kufikia August 2023, Shule za bweni za wasichana za Mikoa zimeanza kudahili wananfunzi ambapo kati ya shule 10 zinazojengwa, shule 7 zimepangiwa wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2023. Aidha, shule 16 kwa mikoa iliyobaki zimeshatumiwa fedha.
  • Shule kongwe 82 zimepanuliwa na 5 kukarabatiwa kuongeza udahili kwa wanafunzi wa kidato cha 5&6;
  • Wizara kupitia TEWW imefanikiwa kusajili wasichana wenye sifa 6,949 waliaacha shule kwa sababu mbalimbali na sasa wanaendelea na masomo yao kwenye vituo vinavyoratibiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima. Wasichana hao kwa sasa wanaendelea na masomo katika vituo 131 vyenye walimu wapatao 803 na mahudhurio yao yanaridhisha na wote wamesajiliwa kwa ajili ya kufanya mtihani wa Maarifa (QT)
  • Wizara kupitia TEWW inaendelea na ukarabati wa vituo 6 na ujenzi wa vituo 8 vitakavyotumika kutolea Elimu kwa Njia Mbadala (Alternative Education Pathway –AEP) kwa wasichana walio nje ya mfumo rasmi. Ujenzi na Ukarabati unaendelea kwenye mikoa 14. Aidha, fedha zimetumwa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano.

 

  1. Uboreshaji kwenye eneo la taaluma
  • Ili kuleta ufanisi katika utoaji wa elimu bora nchini mradi umewezesha utoaji wa mafunzo kazini kwa walimu wapatao 25,109 wa masomo ya Sayansi na Hisabati nchi;
  • Wizara kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania imechapa na kusambaza vitabu vya Hisabati na Sayansi 2,681,800 kwa shule zote za Sekondari nchini.
  • Unaendelea na ununuzi wa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya shilingi bilioni 6 kwa Shule za sekondari 1500 kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji kwa njia ya TEHAMA.
  • Unaendelea na ununuzi wa vifaa vya Maabara vyenye thamani ya shilingi bilioni 5 kwa Shule za sekondari kwa ajili ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya sayansi.
  • Imewezesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Walimu wa shule za Sekondari za Serikali katika kutekeleza mpango wa Shule Salama. Jumla ya walimu 3,294 kutoka katika shule za Sekondari 1,098, Maafisa Elimu Taaluma wa Halmashauri 26, Maafisa Elimu wa mikoa 9, na maafisa elimu wa wilaya kwa mikoa tisa na Maafisa wa idara za Elimu ya Sekondari wa Halmashauri watakaoratibu utekelezaji wa Mpango wa Shule Salama 183.

MAFANIKIO, CHANGAMOTO NA MAPENDEKEZO YA KUTATUA CHANGAMOTO

MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI KWA MWAKA WA FEDHA WA 2022/2023

Utekelezaji wa Mradi wa SEQUIP katika Mwaka wa fedha wa 2022/2023 umekuwa na mafanikio katika maeneo mengi kulingana na viashiria vya utekelezaji vilivyowekwa kama ifuatavyo; -

  • Utekelezaji wa mradi kwa mwaka wa kwanza umefanyika kwa ufanisi ambapo viashiria vyote vya utekelezaji vimefanikiwa kwa asilimia 100.
  • Jumla ya Shule 205 mpya za sekondari za kata kati ya 231 zilizojengwa katika awamu ya kwanza zimeanza kutumika kwa kudahili jumla ya wanafunzi 37,437. Kufunguliwa kwa shule hizi kumesaidia kupunguza msongamano katika shule walizokuwa wanasoma awali na kupunguza umbali wa wanafunzi kutembea kufuata shule. Aidha shule 7 za bweni za mikao zinaanza kupokea wanafunzi wa kidato cha tano mwezo Agost, 2023.
  • Ujenzi wa mabweni na madarasa katika shule za kidato cha Tano na Sita imesaidia kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi katika shule husika.
  • Utekelezaji wa mpango wa Shule Salama unaendelea katika shule za sekondari ambao unasaidia kuongeza ushirikishwaji wa wazazi na jamii katika kusimamia maendeleo ya wanafunzi na shule kwa ujumla. Aidha, wanafunzi wameendelea kufundishwa stadi za Maisha ili kuweza kujilinda dhidi ya changamoto zinazosababisha kuacha shule.
  • Shule za bweni za wasichana za Mikoa zimeanza kudahili wananfunzi ambapo kati ya shule 10 zinazojengwa, shule 7 zimepangiwa wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 2023.
  • Utekelezaji wa mradi umewezesha kupata mavuno ya fedha kwa mwaka wa kwanza ambazo zinatumika kuendelea kutekeleza shughuli za mradi ambapo shule 16 za bweni za wasichana zinajengwa, shule za kutwa 212 na nyumba za walimu 212 (2 in1), ukarabati wa shule kongwe 5, ujenzi wa vyumba vya madarasa 450, matundu ya vyoo 2,220 na mabweni ya wanafunzi 64.

 

CHANGAMOTO KATIKA UJENZI WA SHULE MPYA NA MAPENDEKEZO YA KUYATATUA

Zipo changamoto zimebainika katika utekelezaji wa mradi kama ifuatavyo: -

  • Shule mpya za sekondari zilizoanzishwa hazijapandwa miti. Hivyo walimu na jamii wameelekezwa kusimamia upandaji wa miti katika maeneo yote ya shule.
  • Uchaguzi wa maeneo ya ujenzi usiozingatia utaratibu uliowekwa na gharama za ujenzi zilizopo. Baadhi ya Halmashauri zimependekeza maendeo yenye miinuko, oevu, yaliyojengwa shule nk. Ni vyema Uongozi wa Halmashauri ione umuhimu wa kuchagua maeneo ya ujenzi utakaozingatia kupunguza gharama za ujenzi na maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa shule
  • Migogoro ya Maeneo kati ya wananchi, wataalamu na viongozi wa siasa inayosababisha shule kujengwa katika maeneo ambayo hayazingatii miongozo. Uchaguzi wa maeneo yasiyo na migogoro huleta usalama kwa wanafunzi baada ya shule kukamilika. Uongozi wa halmashauri uhakikishe kuwa maeneo yalitengwa kwa ajili ya shule hazina migogoro