WIZARA YA ELIMU YATOA VIFAA NIT - MILIONI 245 ZATUMIKA

Published on Thursday 08 July, 2021 00:48:51

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa zaidi ya Shilingi milioni 245 kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kwa ajili ya kununua vifaa vya mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege.

 Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya vifaa  hivyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha kuwa mafunzo yanayotolewa katika vyuo yanaakisi  vipaumbele  vya Taifa, mahitaji ya soko, maendeleo ya wananchi, na pia yanakidhi viwango vya kimataifa. 

Amesema Serikali ya awamu ya sita, kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imetoa fedha hizo ambazo zimewezesha kununua vifaa vya kisasa  vya mafunzo ya wahandisi wa matengenezo ya ndege ambavyo vitakidhi mahitaji ya mafunzo ya taaluma hiyo chuoni hapo.

"Vifaa hivi vya mafunzo ni vya kisasa na vyenye ubora wa hali ya juu. Ninaamini kuwa vitakidhi mahitaji ya mafunzo ya taaluma ya uhandisi wa matengenezo ya ndege hapa Chuoni, na tunatarajia vitakiongezea Chuo uwezo wa kutoa elimu bora, hususan kwenye Sekta hii ya kimkakati ya usafiri wa anga," amesema Waziri Ndalichako.

Aidha, Waziri huyo amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa vyuo vya kimkakati kama NIT vinatoa mafunzo yanayoakisi huduma  zinazolenga kuleta maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

Pia ameutaka uongozi wa chuo hicho kuvitunza vifaa hivyo na kuvitumia kwa uangalifu ikiwa ni pamoja na kusimamia kikamilifu matumizi ya vifaa na kuweka utaratibu mzuri wa kuvihifadhi na kuvifanyia marekebisho ili vitumike kwa muda mrefu na kuwezesha kufikia malengo tarajiwa ya Chuo na Taifa kwa ujumla. 

"Ni vyema Mkuu wa Chuo na wasaidizi wako msimamie kikamilifu matumizi ya vifaa hivi na kuweka utaratibu mzuri wa kuvihifadhi na kuvifanyia ukaguzi kwa  kuwa vimegharimu fedha nyingi za walipa kodi, hivyo vinatakiwa kutunzwa vizuri na kutumika vizuri na walengwa ambao ni wanafunzi ili vidumu na kutuwezesha kufikia malengo tarajiwa,"amesema Waziri Ndalichako

Naye Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bahati Geuzye amesema vifaa hivyo vya mafunzo vimenunuliwa kupitia Mfuko wa Elimu unaosimamiwa na TEA baada ya NIT kuwasilisha maombi ya ruzuku  n kukidhi vigezo vya kupata ufadhili huo.

Awali Mkuu wa Chuo cha Taifa cha  Usafirishaji (NIT)  Profesa Zacharia Mganilwa ameishukuru Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia  kwa namna inavyokiangalia chuo hicho cha kimkakati  kwa kukipatia miradi mbalimbali inayolenga kuboresha mafunzo ambayo yatawezesha kutoa Vijana wenye ujuzi na hivyo  kuongeza idadi ya wataalamu katika eneo la Usafiri wa anga.

Akizungumzia vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa na wizara, Profesa Mganilwa amesema vifaa hivyo vitasaidia katika kuimarisha utoaji mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya Ndege ambapo imeongeza kuwa kwa sasa wataalamu wengi katika Sekta ya usafiri wa anga ni kutoka nje ya Tanzania ambapo ametoa mfano takriban asilimia 60 ya marubani  sio Watanzania.

Read 1025 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022