WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUKAMILISHA UJENZI TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI ZANZIBAR

Published on Saturday 10 July, 2021 00:20:33

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeahidi kukamilisha ujenzi wa majengo katika Taasisi ya Sayansi za Bahari
 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyopo Buyu, Zanzibar

Akizungumza baada ya kukagua chuo hicho Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wizara kupitia mradi wa Kuendeleza Elimu ya Juu tayari imeshatenga zaidi ya Shilingi Bilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa mabweni katika Taasisi hiyo.

Waziri Ndalichako amesema mbali ya fedha hizo Wizara imeshaanza kufanya mapitio ya miradi yake ili kuona namna ya kupata fedha za kumalizia ujenzi wa majengo ambayo tayari misingi yake imeshajengwa na imekaa muda mrefu bila kukamilishwa.

"Mbali ya kutenga fedha za ujenzi wa mabweni, lakini mimi na Katibu Mkuu tulishaanza kufanya mapitio  miradi tuliyonayo katika wizara kuona inawezaje kusaidia kukamilisha ujenzi wa majengo yote yaliyoishia katika hatua ya msingi ambayo ni muhimu katika kukamilisha mafunzo," amesema Profesa Ndalichako.

Waziri huyo amesema kwamwe Serikali haiwezi kuona fedha zilizotumika kujenga misingi hiyo zinapotea bure kwa kuwa hakuna fedha za kukamilisha ujenzi. Amesema matamanio yake ni kuona majengo hayo yanaanza kujengwa katika mwaka 2021/22 na kukamilika mwaka 2022/23 ili madhumuni ya kuanzishwa kwa Taasisi hiyo yafikiwe ikiwa pamoja na kutekeleza sera ya uchumi wa bluu.

Aidha, ameupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa kuanza masomo pamoja na kuwa na changamoto mbalimbali, amezisitiza kuwa chuo hicho kinatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  juu ya kuandaa vijana wenye ujuzi ambapo Taassisi hiyo ina Programu za  mafunzo mbalimbali ambayo yanatoa ujuzi katika tasnia ya Sayansi ya Bahari.

Nae Mbunge wa Kiembe Samaki  ambapo Taasisi hiyo ipo Mhe. Mohammed Maulid amemshukuru Waziri kwa kufika katika Taasisi hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwa taifa katika kuandaa wataalamu wa sayansi ya majini ambao wataiwezesha kufanikisha uchumi wa bluu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari Dkt.Magreth Kyewalyanga amemwambia waziri kuwa ili kukamilisha ujenzi wa miundombinu iliyo kwenye hatua ya msingi zinahitajika kiasi cha shilingi bilioni saba  na milioni mia tano.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Serikali ya wanafunzi DARUSO Frank Buluma amesema Taasisi hiyo imewasaidia wao kama vijana kupata fursa  ya kupata elimu ya Sayansi  ambayo itawawezesha kushiriki katika kukuza uchumi kupitia uchumi wa bluu. Ametoa wito kwa vijana kujiunga na chuo hicho ambacho kitawawezesha kupata elimu itakayowasaidia kujiajiri katika eneo jipya la ajira.

Taasisi ya Sayansi za Bahari, inatoa mafunzo katika ngazi umahiri, uzamivu na shahada za awali,  kufanya tafiti na kutoa ushauri katika maeneo mbalimbali ya Sayansi ya Bahari.

Read 1330 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022