Waziri wa Elimu ya Msingi kutoka Afrika Kusini Matsie Angelina Motshekga Julai 5, 2022 amefanya ziara katika Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko iliyopo jijini Dar es Salaam ili kujionea uendeshaji wa mfumo wa utoaji mafunzo Jumuishi katika ngazi ya elimu ya msingi.
Akiwa shuleni hapo Waziri huyo amefurahishwa na namna shule hiyo inavyoweza kutoa elimu jumuishi kwa kuweze kuwa na wanafunzi wote kushiriki ujifunzaji katika darasa moja.
Waziri Motshekga amesema changamoto kubwa iliyopo nchini mwao ni kutokuwa na mfumo jumuishi jambo ambalo linapelekea wazazi kuona watoto wenye mahitaji maalum wananyanyapaliwa.
"Nimefurahi sana kuona namna mfumo elimu jumuishi unavyoendeshwa katika shule hii, nimepata funzo kubwa sana hapa ambalo tunakwenda nalo, kwetu tumekuwa tukiwatenga watoto wenye mahitaji maalum na kuonekana tunawanyanyapaa," amesema Waziri huyo
Aidha, amewapongeza walimu wa shule hiyo kufundisha watoto hao kwa upendo na kupelekea watoto kuwa na furaha wanapokuwa shuleni.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa (TAMISEMI) David Silinde amesema pamoja na Waziri huyo wa Afrika Kusini kujifunza namna elimu Jumuishi inavyoendesha, pia Tanzania inajifunza namna nchi hiyo ilivyofanikiwa kuifanya lugha ya alama kuwa ya lazima katika ngazi zote za elimu.
Naibu Waziri Silinde amesema anaichukua hiyo na wataijadili na viongozi wengine wa elimu kuona namana Serikali inavyoweza kuifanya lugha ya alama kufundishwa nchini kwa wanafunzi wa ngazi zote.