WAZIRI NDALICHAKO AMEZITAKA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA KUFANYA KAZI KWA WELEDI.

Published on Monday 11 October, 2021 11:39:42

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara kufanyia kazi  kikamilifu yale yote ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiyasemea katika hotuba zake, maelekezo na mipango ya Taifa kwa kuwa ana lengo la kuendelea kujenga uchumi na kuondoa kero za wananchi.

Waziri Ndalichako amesema hayo Jijini Dar es Salaam katika kikao cha Mawaziri wa Elimu Bara na Zanzibar na Watendaji pamoja na Bodi ya Tume ya Taifa ya UNESCO na kuzitaka Taasisi zote kutekeleza majukumu yake kwa wakati na weledi mkubwa kwa lengo la kutoa matokeo chanya.

“Tunamshukuru sana Mhe Rais kwa kutoa kipaumbele kwenye elimu, ametoa fedha ambazo zitawezesha kujenga madarasa elfu 15 kwa mpigo, madawati zaidi ya laki nne kwa mkupuo,  kukamilisha VETA  32, kujenga kumbi za mihadhara kwenye vyuo 17 vya ualimu, kununua vifaa vya kufundishia kwenye vyuo vya maendeleo ya wananchi, kuongezea vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa watoto wenye mahitaji maalum, lakini pia tunaendelea kunufaika kupitia sekta nyingine kama  maji yatakapowekwa kwenye mikoa wilaya hakuna shaka shule  na Vyuo vyetu vitanufaika ” amesema Prof. Ndalichako

Akizungumzia majukumu ya Tume ya Taifa ya UNESCO Mhe. Ndalichako amesema Tume hiyo ina majukumu mengi na mapana ikiwemo kusimamia amani ya dunia na kwamba katika kipindi hiki ambacho Mhe. Rais anasisitiza masuala ya amani, umoja na utulivu ni vizuri Tume hiyo ikafahamu kwamba hilo pia ni jukumu lao kwani huwezi kuwa na amani ya dunia kama hakuna amani ya taifa moja moja.

“Nafahamu mnakuwa na program ambazo zinaanzishwa kwa ajili ya wanawake, vijana, viongozi wa dini, wanasiasa na wahabari zenye lengo la kutoa elimu ambayo inahamasisha amani na usalama kwa maslahi mapana ya nchi, ni vizuri mkajua mna jukumu la kuendelea kuhamasisha na kulinda amani na utamaduni wetu,” amesema Mhe. Ndalichako

Pia Mhe. Ndalichako amewakumbusha wajumbe wa Bodi ya Tume ya UNESCO kuwa wana jukumu la kuendelea kuangalia maeneo ya utalii yanayoendana na urithi wetu yanayofaa kutambulika kwani Mhe Rais sasa anaendelea kusisitiza suala la utalii  kwani ni moja ya sekta muhimu ambazo zinaniua uchumi wetu.  

“Mhe Rais amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu kupitia Royal Tour ameonesha njia, sasa Mwenyekiti tumuunge mkono Rais wetu sisi kama Tume ambayo tumepewa jukumu la kuangalia hayo maeneo kuhakikisha yanahifadhiwa vizuri, kuyafanyia tathmini kwa weledi kama bado yapo kwenye hadhi yake tukitambua yana mchango katika kuongeza utalii katika nchi yetu lakini kuifanya nchi kujulikana katika ramani ya Dunia kutokana na vivutio vilivyopo,” amesema Waziri Ndalichako

Aidha Mhe. Ndalichako ameitaka Bodi ya Tume ya UNESCO kuhakikisha Tume inajitangaza kazi inazofanya, ili tuweze kutambulika na mchango wake kuonekana ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Simai Mohamed Said (Mb) amesema ni vizuri Bodi ya Tume ya UNESCO kuangalia maeneo ya urithi na kuweza kuishauri Serikali ili kuyaweka maeneo hayo katika urithi wa nchi yetu kwani yakiachwa yanaweza kupotea na kufutika katika urithi wa nchi yetu.  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya UNESCO Prof. Elifaz Tozo Bisanda amemuahidi Waziri Ndalichako kuwa Bodi anayoisimamia itafanyia kazi maelekezo yote aliyotoa ikiwemo kutangaza Tume ya UNESCO ili  ijulikane pamoja na kuendela  kusimamia majukumu mengine yote ya Tume kulingana na maelekezo ya viongozi hao.

Read 447 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top