WAZIRI MTEULE WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA PROF. MKENDA AKABIDHIWA OFISI RASMI

Published on Thursday 13 January, 2022 14:55:30

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema atatumia wataalam wa elimu wa ndani na nje ya wizara  ili kuwa na maamuzi yenye tija kwa nchi.

Waziri Mkenda amesema hayo leo Januari 13, 2022 jijini Dodoma wakati  akikabidhiwa ofisi  na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo Profesa Joyce Ndalichako ambapo ameongeza kuwa katika uongozi wake hatatoa maamuzi juu ta sekta ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu bila ya kushauriana na wataalam husika katika sekta hiyo.

Profesa Mkenda amesema anafanya hivyo kwa kuwa  Wizara hiyo inahitaji utulivu  na siyo ya kubadilisha mambo ama kutoa matamko bila kuzingatia maoni ya wataalam kwani kufanya hivyo ni kuwachanganya wananchi.

"Kabla ya kufanya maamuzi yoyote katika elimu lazima kuwe na mijadala mipana iliyo huru kwa kutumia wataalamu wa ndani na nje ya wizara ili tuwe na maamuzi ya pamoja yenye tija," amesema Prof. Mkenda

Waziri huyo ameendelea kuwasisitizia watumishi wa wizara hiyo na watalaam wa elimu waliopo wizarani kutoa maoni walionayo, kufanya kazi kwa ujasiri, nidhamu na kujiamini na kwamba linapokuja suala la ubora wa elimu anawategemea.

Akizungumza katika halfa hiyo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema  wizara ya elimu ni kubwa ambayo inashughulika na wananchi  moja kwa moja na hivyo inahitaji umakini.

Amesema  pia ipo Miradi  iliyoleta Tija ambayo ni pamoja na  Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)  ambao katika awamu ya kwanza tu ambayo imekamilika Mwezi Desemba 2021umeacha alama kwa watanzania kwani umegusa kila kona ya nchi kwa kujenga miundombinu mbalimbali ya Elimu.

Prof. Ndalichako amemwambia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwa Mwezi Desemba Benki ya Dunia imeidhinisha mkopo wa Dolla Milioni 500 ambayo ni zaidi ya shilingi trioni moja kwa ajili ya kuimarisha elimu msingi

Amesema pamoja na fedha hizo lakini bado wizara ina fedha zaidi ya Trioni tatu ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi na kwamba yeye atakuwa tayari pale atakapohitaji ushauri wowote.

Makabidhiano hayo yamefanyika ikiwa ni siku chache tangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ameliapisha Baraza la Mawaziri.

Read 877 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top