Waziri Mkuu Majaliwa asisitiza ufundi stadi kuwezesha ajira kwa Watanzania

Published on Tuesday 30 November, 2021 07:30:04

Waziri Mkuu Ka ssim Majaliwa amesema Serikali imejipanga kuwapatia ujuzi Watanzania kupitia mafunzo ya ufundi stadi ili waweze kujiajiri na kuajiriwa.
 
Akizungumza wakati wa kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha ufundi stadi cha Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya  tarehe 29 Novemba, 2021, Mhe. Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imefanya uamuzi wa kujenga vyuo vya ufundi stadi nchini ili wananchi hususani vijana wapate ujuzi na ufundi wa aina mbalimbali na kuweza kushiriki shughuli za kiuchumi na kujipatia kipato.

Mhe. Majaliwa ameagiza ujenzi wa Chuo cha VETA Chunya ukamilike kwa wakati ili malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya ufundi chuoni hapo yanafikiwa huku akiwataka wananchi kuendelea kuwa na imani na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali.
 
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga, amesema kwa sasa Serikali inajenga vyuo vya VETA kwenye Wilaya 29 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 48.8 zimeshatumika  kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo.

Mhe. Kipanga amesema kiasi kingine cha shilingi bilioni 64 kimetolewa na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo hivyo pamoja na kuwezesha ujenzi wa vyuo vingine vinne vya mikoa ya Geita, Simiyu, Rukwa na Njombe.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu amesema ujenzi wa chuo hicho ulianza mwezi Machi, 2020 na kwamba mradi huo una jumla ya majengo 17 ambayo ni jengo la utawala, karakana nne, jengo la madarasa, mabweni mawili, bwalo la chakula, majengo matatu ya vyoo, nyumba ya mkuu wa chuo, nyumba ya familia mbili za watumishi, jengo la mitambo ya umeme, jengo la stoo na jengo la walinzi na kuwa  kinatarajiwa kudahili wanafunzi 720 kwa mwaka.

Read 343 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top