WARATIBU WA MIRADI YA SWASH WAPEWA MAFUNZO KUBORESHA UTENDAJI

Published on Monday 12 July, 2021 22:48:12

Jumla ya Waratibu 103 wa miradi ya Huduma za Maji, Elimu ya Afya na Usafi wa Mazingira (School Water, Sanitation and Hygiene -  SWASH) wakiwemo 17 wa Mikoa na 86 wa Halmashauri wanashiriki mafunzo ya siku tano kuhusu Mwongozo wa SWASH  mkoani Morogoro.

Akifungua mafunzo hayo Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Gerald Mweli amesema yanalenga kuwajengea uwezo Waratibu hao katika kusimamia na kuratibu huduma bora za maji, elimu ya afya na usafi wa mazingira.

Naibu Katibu Mkuu Mweli amesema anaamini kuwa baada ya mafunzo hayo Waratibu watapata ujuzi na uelewa mkubwa wa programu utakaowawezesha kusimamia utekelezaji wa miradi kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuweza kupata fedha za kujengea vyoo vingine.

“Vyoo vinavyojengwa si kwa ajili ya wanafunzi tu! bali hata walimu pia, hivyo tujenge kwa viwango bora ili tuweze kupata fedha za kuhudumia shule nyingi zaidi,” amesema Mweli.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amewaagiza Waratibu hao kusimamia matumizi ya fedha za miradi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na miongozo ya fedha ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya force account; na kushirikisha Wahandisi wa Halmashauri ili kuhakikisha miundombinu inayojengwa inakuwa na viwango vya ubora vinavyokubalika.

Mweli amewataka pia Waratibu hao kuhakikisha shule zote za msingi zinakuwa na Vilabu vya Usafi wa Mazingira Shuleni (School Wash Clubs) na zinakuwa na mwalimu wa kike anayeshughulikia masuala ya hedhi salama kwa ajili ya kusimamia afya ya hedhi shuleni.

Read 1473 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022