Watumishi wanawake wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wamehitimisha siku ya wanawake duniani kwa kutoa msaada wa vifaa kwa wanafunzi viziwi wa Shule ya Msingi Kigwe iliyopo Wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma.
Akizungumza leo Machi 11, 2023 mara baada ya kukabidhi vifaa hivyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo Bi. Sylvia Lupembe amesema kilichofanyika ni upendo na kurudisha kwa jamii kile kidogo walichonacho.
"Ndugu zangu katika kuhitimisha siku ya wanawake duniani tumeona tulete kidogo tulichojaliwa kwa watoto wetu hawa na kupata muda wa kuzungumza nao. Tunatambua elimu bora ni kwa watoto wote na kama mama, walezi tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa wote"
Ametaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni magodoro, simtank kwa ajili ya maji, taulo za kike, mpira wa michezo kwa wanafunzi wa kike na kiume, mashuka, na viburudisho ikiwemo biskuti, maji, juisi na keki.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kigwe Adon Mabakwe amewashukuru wanawake wa Wizara ya Elimu kwa kujitoa kwa ajili ya wanafunzi hao ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Nae Afisa elimu Elimu Maalum Halmashauri ya Wilaya ya Bahi Sarah Chizingwa ameshukuru watumishi wanawake wa Wizara ya Elimu kwa upendo waliouonesha wa kuwatembelea wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Kigwe Thadei Mhwagila amewashukuru watumishi wanawake kwa kuwatia moyo kwa zawadi kwani ni kubwa na zitasaidia sana kupunguza changamoto zilizokuwepo, huku akiomba wizara kuwapatia vifaa vya Tehama kwa ajili ya ujifunzaji.