Wanafunzi wa SUA wanufaika na Mafunzo kwa vitendo 

Published on Tuesday 21 March, 2023 11:54:14

Wanachuo 186 wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Morogoro, wameshiriki  mafunzo kwa vitendo yanayohusiana na utunzaji na uhifadhi wa mifumo ya kiikolojia ya mwambao wa Pwani na maji chumvi (coastal and marine ecosystems) kwenye Pwani ya Tanzania. Pamoja na mambo mengine, wanachuo hao wamejifunza kuhusu ikolojia ya misitu ya mikoko yenye eneo la hekta 28 katika Wilaya ya Ilala Mkoani Dar es Salaam.

Wanachuo hao ni wa mwaka wa kwanza katika Shahada ya Sayansi za Mazingira na Usimamizi wa Mazingira kwa mwaka wa masomo 2022-2023. Mafunzo ya kiikolojia yamefanyika tarehe 13 Machi 2023 kwenye eneo la lango la mto Msimbazi karibu na daraja la Salenda jijini Dar es Salaam. 

Wamejifunza aina mbalimbali za mikoko ambako hasa aina kumi zinazopatikana kwa wingi kwenye ukanda wa Pwani ya Tanzania. Aina hizo ni mkaka, mkandaa, msinzi, mchu, mpira, msikundazi, mkomafi mweupe, mkandaa dume, na mseji. Wanachuo walipata fursa ya kuona, kuitambua na kujifunza kuhusu umuhimu wa mikoko kiikolojia, kwa viumbe wengine pamoja na binadamu. 

Akifundisha Wanachuo hao Afisa Mhifadhi Mkuu Frank Sima kutoka Wakala wa Misitu Nchini (TFS), Wizara ya Maliasili na Utalii, alielezea kuwa mikoko ina faida kubwa za kiikolojia kama vile kuwa sehemu ya mazalia na unenepeshaji wa samaki aina mbalimbali hasa samaki kaa, kuzuia mmomonyoko wa udongo utokanao na mawimbi ya bahari na upepo, kufyonza hewa ukaa kwa kiwango kikubwa kuliko miti ya aina zingine, utalii wa kiikolojia, ufugaji nyuki. Mikoko inachangia katika kuchuja aina mbalimbali za takataka ngumu, na kikemikali ili zisiingie baharini.

Aidha, Mhahiri Mwandamizi Dkt. Elly J. Ligate kutoka Idara ya Elimu ya Viumbe Hai (Biosciences) ya SUA, aliyeongozana na wanachuo hao, amesisitiza kwamba ni muhimu wanachuo hao wakawa mabalozi kwa kuwaelimisha Watanzania wengine kuhusu umuhimu wa mfumo wa kiikolojia ya mwambao wa Pwani na maji-chumvi katika afya ya mazingira, ikolojia, maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.

 Amewaasa Watanzania kupunguza uharibifu wa mifumo ya kiikolojia na kutotupa taka katika mifumo hiyo. Kwa kipindi kirefu sasa Dunia inashuhudia madhara yatokanayo na uharibifu wa mazingira ikiwa hasa kuongezeka kwa joto duniani, kuongezeka kwa vimelea vya maradhi na milipuko ya magonjwa kwa sababu afya ya mazingira imetoweka” Amesema Dkt Ligate.

Naye mtaalamu wa elimu ya mimea kwa vitendo Bwana Gaston Mbilinyi, amewaasa wanachuo hao kuzingatia mafunzo yanayotolewa kwani wamepata nafasi adimu ya kuona na kutenda
Amesema Bw. Mbilinyi.

Nao Viongozi wawakilishi wa wanafunzi Simkoko, Yusuph, Mwambelo na Upendo wamekiri kuwa mafunzo kwa vitendo yamewafungua macho na ufahamu kuhusu uhalisi wa mambo waliyo yasoma kinadharia chuoni. “Wapo wenzetu wengi katika darasa hili, ndiyo wameiona bahari, maji bahari na viumbe bahari kwa mara ya kwanza siku ya leo” anasimulia mmoja wa wanachuo hao.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  huendesha mafunzo kwa vitendo kila mwaka kwa kutembelea maeneo ya hifadhi za ukanda wa pwani na maji chumvi hasa kujifunza manufaa, umuhimu na utunzaji wa mikoko ya Mkoa wa Dar-es-Salaam katika wilaya za Ilala, Kinondoni, Temeke, na Kigamboni.

Read 348 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top