VETA kushirikiana na Ujerumani kuwezesha wahitimu kupata ajira

Published on Wednesday 18 September, 2019 05:09:31

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imeingia makubaliano na Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ) kuboresha hali ya upatikanaji wa ajira kwa wahitimu wa Ufundi stadi kupitia mradi  uliopewa jina la Ajira kwa Maendeleo.

Mradi huo unalenga katika kutambua mahitaji ya ujuzi katika viwanda na makampuni mbalimbali yanayowekeza kwenye mikoa ya kusini na kuingiza ujuzi huo katika mafunzo ili hatimaye kutoa wahitimu watakaoajirika kwa urahisi.

Akizungumza wakati wa kutia saini makubaliano hayo Dar es Salaam jana Septemba 17, 2019 Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu alisema kuwa mradi huo utatekelezwa kupitia Chuo cha VETA Lindi ambapo GIZ imeajiri mtaalamu ambaye atatumika kutoa ushauri kwa uongozi wa chuo, walimu na wanafunzi juu ya namna ya kuwezesha wahitimu wa chuo hicho kujipatia ajira mara wanapohitimu.

Alisema ushirikiano huo utaboresha mahusiano kati ya chuo cha VETA Lindi na waajiri ambapo wanafunzi wataweza kupatiwa nafasi za mafunzo kwa vitendo na kufundishwa juu ya mbinu mbalimbali za kuajirika na kujiajiri na hata kuunganishwa na nafasi za kazi katika makampuni mbalimbali.

Naye Msimamizi wa Masuala ya Ufundi Stadi wa GIZ Iris Rotzoll alisema kuwa GIZ imeamua kushirikiana na VETA ili kuwezesha vijana wanaohitimu katika chuo cha VETA Lindi kutumia vizuri fursa za ajira zinazopatikana kutokana na uwekezaji unaoendelea kufanyika katika mikoa ya kusini mwa Tanzania hususani makampuni ya uzalishaji, uchakataji na usafirishaji wa gesi.

Alisema ushirikiano huo umekuja kutokana na mafanikio yaliyojitokeza chini ya Mradi wa Kuongeza sifa za Kuajiriwa kupitia mafunzo ya Ufundi ujulikanao kama EEVT uliokuwa ukitekelezwa na VETA, VSO Tanzania na Makampuni ya gesi chini ya mwavuli wa LNG kuanzia mwaka 2012 hadi 2018 ambapo jumla ya vijana 1,027 waliwezeshwa kuboresha ujuzi wao kwa viwango vya kimataifa huku wengi wao wakipata ajira kwenye miradi ya Kimataifa inayotekelezwa hapa nchini.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha VETA Lindi Mhandisi Cleophas Sikada alisema kuwa ushirikiano huo utasaidia pia kuboresha utoaji ushauri wa kitaaluma kwa wanafunzi na kuboresha kanzi data ya wahitimu wa ufundi stadi pamoja na waajiri.

Alisema chuo cha VETA Lindi kitashirikiana kwa karibu na mtaalamu huyo ili kuhakikisha kuwa mradi huo unanufaisha walimu, wanafunzi na wahitimu wa chuo hicho.

Read 1951 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top