UJENZI VYUO 25 VYA VETA WILAYA NA 4 VYA MIKOA KUKAMILIKA MWAKA HUU WA FEDHA

Published on Friday 15 October, 2021 23:40:40

Serikali itatumia Shilingi bilioni 51 katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kumalizia ujenzi vya Vyuo 25 vya VETA vya Wilaya, vyuo 4 vya mikoa ya Njombe, Simiyu, Geita na Rukwa pamoja na upanuzi wa vyuo vingine vya mikoa.

Hayo yamesemwa hivi karibuni Mkoani Mtwara na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omari Kipanga (Mb) wakati akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Wilaya ya Masasi ambapo amesema fedha hizo zitaanza kusambazwa kwenye miradi husika baadae mwezi huu ili kuwezesha miradi hiyo kukamilika kwa wakati.

"Niwatoe hofu ndugu zangu, fedha hizi zipo kwahiyo tumejizatiti kuhakikisha tunakamilisha hizi VETA ikiwemo hii ya Mtwara ili kuongeza Vijana wenye ujuzi," amefafanua Mhe. Kipanga.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kipanga amewataka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kutoa mafunzo ya taaluma zinazoendana na shughuli za kiuchumi wa eneo husika ili iweze kuwasaidia wanajamii wa eneo hilo kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuweza kuzalisha zaidi.

"Kama shughuli kubwa ya mazingira ya hapa ni ubanguaji korosho, ni vizuri mkatoa mafunzo ya ubanguaji korosho, hii itasaidia zaidi kuwakwamua wanajamii kutoka kwenye wimbi la umaskini. " amefafanua Mhe. Kipanga.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkuu wa VETA Mtwara ambao ndio wasimamizi wa mradi huo, Joseph Kibehele amesema ujenzi wa chuo hicho ulianza Januari 2020 na unatarajia kukamilika Desemba 2021 na kwamba mpaka sasa ujenzi umefikia asilimia 81.

Amesema chuo hicho chenye eneo la ukubwa wa ekari 50 kitagharimu Shilingi bilioni 2.3 hadi  kukamilika na kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa wanachuo 240 wakiwemo 144 wa bweni. Pia kitaweza kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa washiriki zaidi ya 950 kwa mwaka.

Kibehele amesema chuo hicho kitakuwa na majengo 17 yakiwemo mabweni ya wasichana na wavulana, maabara, madarasa, maktaba, jengo la utawala, nyumba za watumishi, jiko, bwalo la chakula, karakana, jengo la mlinzi na jengo la mtambo wa umeme.
[11:01 am, 15/10/2021] Ipyana Moest: Muonekano wa baadhi ya majengo yanayojengwa katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Read 383 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top