ufungaji wa mafunzo ya TEHAMA na Teknolojia Saidizi kwa wakufunzi na walimu wa Sekondari wenye mahitaji maalum

Published on Thursday 06 February, 2020 14:24:06

SERIKALI imesema itaendelea na mpango mkakati wa kutekeleza elimu bila malipo pamoja na kutoa vipaumbele kwa watu wenye ulemavu kupata elimu iliyo bora.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.Ave Maria Semakafu wakati wa ufungaji wa mafunzo ya TEHAMA na Teknolojia Saidizi kwa wakufunzi na walimu wa Sekondari wenye mahitaji maalum.

Dk. Semakafu amesema serikali imejipanga kuhakikisha walimu na wanafunzi wanapata elimu ya Tehama, elimu jumuishi sambamba na kujenga shule zao maalum katika kila mkoa ambapo kwa sasa wameanza na mkoa wa Katavi.

Hata hivyo awali ilielezwa kuwa tayari serikali imetumia kiasi cha shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya kununua na kusambaza vifaa maalum vya kielimu saidizi katika shule za msingi na sekondari zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum nchini.

“Hii kazi pia si ndogo, napenda kwa namna ya kipekee kabisa kutumia nafasi hii kuushukuru Uongozi wa Chuo Kikuu Huria kwa kukubali kuendesha mafunzo haya hapa chuoni na kutoa wawezeshaji, vifaa pamoja na miundombinu mingine kwa ajili ya kufanikisha mafunzo haya muhimu,’’ amesema Dk. Semakafu.

Aliongeza kuwa mafunzo waliyoyapata ni muhimu kwani yatawasaidia katika matumizi ya TEHAMA kwenye ufundishaji na ujifunzaji, kutafuta rejea mbalimbali za kielektroniki kwenye mitandao na kutumia teknolojia saidizi zinazowezesha matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo, Mwalimu wa shule ya sekondari ya Binti Mussa iliyopo Kiwalani jijini Dar es Salaam, Anna Mbogo alisema wanaishukuru kwa dhati Wizara ya Elimu kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa walimu wenye mahitaji maalum.

“Mafunzo haya yalilenga kutujengea uwezo sisi walimu kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ya sasa, pia tunaushukuru uongozi wa OUT chini ya serikali ya awamu ya tano kuonesha bayana nia ya kuwasaidia walimu wenye mahitaji maalum na kuwathamini watu wenye ulemavu kwa kuajiri watu wenye ulemavu,’’ amesema Mwalimu Anna

Read 1640 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022