TAARIFA KWA UMMA
UFAFANUZI KUHUSU UTEKELEZAJI WA WARAKA WA ELIMU NA. 01 WA MWAKA 2023 NA WARAKA WA ELIMU NA. 02 WA MWAKA 2023
24 Machi, 2023
DODOMA
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia kwa Kamishna wa Elimu, ilitoa Waraka wa Elimu Na. 01 wa mwaka 2023 unaohusu Uboreshaji wa Huduma za magari/mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi na Waraka wa Elimu Na. 02 wa mwaka 2023 kuhusu Utoaji wa Huduma ya kulaza wanafunzi Bweni kwa ngazi za Elimu ya Awali na Msingi.
Wizara inatoa taarifa kuwa Waraka Na. 2 kuhusu Utoaji wa Huduma ya Kulaza bweni wanafunzi chini ya darasa la tano haujafutwa. Waraka huo ni msisitizo wa Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule wa Mwaka 2020. Wadau wote wanapaswa kuzingatia Waraka huu. Hata hivyo, kama Waraka Na. 2 wa Mwaka 2023 ulivyoelekeza, watakaoruhusiwa kupokea wanafunzi chini ya darasa la tano katika shule za bweni ni wale tu watakaopewa kibali maalum na Kamishna wa Elimu. Kwa hiyo wale wote waliokuwa na kibali cha Kamishna kwa sasa hawahusiki na katazo hili. Mchakato wa kuchambua suala hili na kuchukua maamuzi zaidi utafanywa kwa kushirikisha kikamilifu wadau wote.
Pia inafahamishwa kuwa utekelezaji wa Waraka Na. 1 wa Mwaka 2023 kuhusu Uboreshaji wa Huduma za magari/mabasi yanayotumika kusafirisha wanafunzi uko pale pale isipokuwa kwenye suala la kuajiri wahudumu wa mabasi wenye jinsia ya kike na kiume. Muda wa kuanza utekelezaji wa suala hili umesogezwa mbele kwa sasa ili kupisha majadiliano na wadau kupanga namna bora ya kutekeleza suala hilo la ajira za wahudumu wa magari/mabasi ya wanafunzi.
Imetolewa na:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI