SHULE ZENYE CHANGAMOTO YA MIUNDOMBINU KUNUFAIKA NA MFUKO WA ELIMU WA TAIFA

Published on Friday 05 August, 2022 22:56:27

Shule zenye uhaba mkubwa wa miundombinu unaotokana na kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi na zilizosajiliwa zinatarajia kunufaika na Mfuko wa Elimu wa Taifa unaosimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Hayo yameleezwa Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Idara ya Habari - MAELEZO kuhusu utekelezaji na mwelekeo wa Bajeti ya TEA kwa mwaka 2022/23.

Amesema TEA imepanga kutumia kiasi cha Sh. Bilioni 8.9 kwa ajili ya kufadhili miradi ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambapoTaasisi mbili za elimu ya juu za Tanzania Zanzibar pamoja na shule zilizo na changamoto za miundombinu zitanufaika.

Ametaja Taasisi za elimu ya juu zitakazonufaika kuwa ni Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia Zanzibar (KIST) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA)   ambapo  jumla ya Sh Milioni 500  zitatumika. 

“Tunaendeleza jitihada za Serikali kuwezesha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini, tutatumia Sh bilioni 8.9 kwa ajili hiyo na kujenga jumla ya miradi 96 katika shule za msingi na sekondari Tanzania bara pamoja na Taasisi mbili za elimu ya juu Tanzania Zanzibar. Shule zitakazonufaika ni zenye vigezo ambavyo vimetajwa pamoja na kuwepo kwenye kanzi data ya TEA,” amesema Bibi Geuzye

Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa 99, matundu ya vyoo 792, maabara 10 za masomo ya sayansi kwa ajili ya shule tano za sekondari, nyumba za walimu 52 na mabweni 10. 

Miradi mingine ni ujenzi wa miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum inayojumuisha madarasa 10, matundu ya vyoo 40 pamoja na mabweni mawili katika shule sita zenye watoto wenye mahitaji maalum. 

Awali Mkurugenzi Geuzye alisema TEA katika mwaka wa fedha 2021/2022, ilitumia kiasi cha Sh. Bilioni 8.6 kufadhili miradi 160 ya kuboresha miundombinu ya elimu katika shule 151 nchini. Miradi hiyo ilijumlisha ujenzi wa madarasa 210 katika shule 70, Maabara 2 za sayansi katika shule za sekondari zenye mahitaji maalum, Matundu ya vyoo 1920 katika shule 80, vifaa vya kujifunzia na kufundishia na uendelezaji wa   miundombinu  katika shule  tisa za watoto wenye mahitaji maalum pamoja na ofisi mbili za walimu katika shule mbili.

Aidha Mkurugenzi  Geuzye ameendelea kuhimiza wadau wa elimu kutoa  ufadhili  wa miradi ya elimu kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao una jukumu la kisheria la kuratibu  michango  inayotolewa katika sekta ya  elimu nchini ili kuwezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za  wachangiaji na thamani ya michango.

“Taasisi au watu wanaochangia kupitia TEA wanatambuliwa rasmi kwa kupewa cheti maalum na wanaweza kuomba nafuu ya kodi kwa Kamishna wa Kodi ya Mapato Nchini (TRA). Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001 na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mapato ya mwaka 2006,” alisema Mkurugenzi Geuzye. 

Kuhusu utekelezaji wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), Mkurugenzi Mkuu wa TEA amesema hadi kufikia mwezi Juni 2022 kiasi cha Shs   Bilioni 9.7 zinatumika kufadhili miradi 81 ambapo  jumla ya wanufaika 33,510 ikiwa ni wanaume 17,257 (51.5%) na wanawake 16,253 (48.5%) wamepatiwa mafunzo.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa. Pia TEA inaratibu Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.

Read 1613 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top