SHULE NA VYUO ZATAKIWA KUFUATA MWONGOZO WA KUJIKINGA NA MAAMBUKIZI YA KORONA (COVID - 19)

Published on Thursday 28 May, 2020 21:52:33

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, amezitaka Shule kuacha kutumia ugonjwa wa Covid-19 kama kitega uchumi kwa kuagiza fedha za ziada kutoka kwa wazazi; na kuwa Serikali itachukua hatua kwa shule zinazofanya hivyo ikiwa ni pamoja na kuzifutia usajili.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo jijini Dodoma alipozungumza na Vyombo vya Habari kuhusu Mwongozo wa Kudhibiti Maambukizi ya Ugonjwa wa Corona (Covid-19) katika Vyuo na Taasisi za Elimu nchini uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.

Amesema baadhi ya shule zimekuwa zikitoa maelekezo mbalimbali kwa wanafunzi wakati huu wa kuelekea kufungua shule, ikiwa ni pamoja na kuwaagiza wanafunzi kubeba lita mbili za spiriti, limao za unga na tangawizi, huku wengine wakiweka michango isiyokuwa na uhalali wowote.

“Wanafuzi walikuwa wameshalipa ada kabla ya kufunga shule na walikwenda nyumbani kwa kuwa kulikuwa na changamoto ya mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona. Baada ya kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali, hali ya maambukizi imepungua. Ndio maana shule na vyuo vinafunguliwa na wanafunzi wanakwenda kuendelea walipoachia kwa fedha zao walizolipa. Hakuna malipo ya ziada,” amesisitiza Prof. Ndalichako.

Amezitaka shule kuendelea kuwapa wanafunzi vyakula vinavyowapa vitamin ‘C’ badala ya kuwatuma wanafunzi kuleta vitu ambavyo ni vya kutengenezwa.

Pia amesisitiza shule na vyuo kuzingatia mwongozo wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona uliotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

“Ni marufuku kwa
wanafunzi kwenda na spiriti shuleni kwani inaweza kuchoma shule na mabweni na pia inaweza kutumika kama kilevi.”

Read 3775 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top