SERIKALI YAZINDUA MWONGOZO WA CHAKULA NA LISHE KWA WANAFUNZI WA ELIMUMSINGI

Published on Sunday 31 October, 2021 00:59:55

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Oktoba 29, 2021 imezindua Mwongozo wa Kitaifa ya Utoaji Huduma ya Chakula na Lishe kwa Wanafunzi wa Elimumsingi wenye lengo la kuwaelekeza wadau wa elimu nchini namna bora ya kutekeleza utoaji huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi.

Akizindua Mwongozo huo Jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Leonard Akwilapo amesema Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 imetamka wazi kuwa utoaji wa huduma muhimu kama chakula bora, maji safi na upatikanaji wa huduma za afya kwa wanafunzi wawapo shuleni ni muhimu. Hivyo Wizara imeandaa Mwongozo wa kisera ili kuweka utaratibu wa Kitaifa utakaonufaisha shule na wanafunzi wote wa Elimumsingi nchini.

Dkt. Akwilapo amesema mwanafunzi anapokosa chakula shuleni anaweza kupata madhara ikiwemo  kukosa usikivu wakati wa ujifunzaji, mahudhurio hafifu yanayopelekea utoro na hata kukatisha masomo na kushuka kwa ufaulu.

"Natambua kwamba utoaji wa huduma ya chakula na lishe ni suala mtambuka linalohitaji ushiriki wa sekta na wadau mbalimbali. Ni matumaini yangu kuwa kila mmoja atasoma Mwongozo huu na kutekeleza majukumu yake ipasavyo," amesema Dkt. Akwilapo.

Aidha, Katibu Mkuu Akwilapo ametoa rai kwa idara zote za Serikali na Wizara zinazohusika na jukumu hili kuhakikisha zinasimamia utekelezaji wa Mwongozo huo na kutoa wito kwa wadau wote wa Elimu kushiriki, kuchangia kwa hiari na upatikinaji wa chakula  chakula bora kwa watoto wanapokuwa shule i.

"Niwaombe wadau wetu wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, makampuni binafsi na vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha ili kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata chakula wanapokuwa shuleni," amesisitiza Dkt. Akwilapo.

Akiongea baada ya uzinduzi wa Mwongozo huo, Katibu Mkuu TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe ameziagiza Sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa kutekeleza mwongozo huo kwa ufanisi na kuwataka ambao wamekuwa wakitoa huduma za chakula shuleni kuendelea kutoa huduma hiyo kwa kuzingatia Mwongozo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Project Concern International (PCI), Nicholaus Ford amesema Shirika hilo linatekeleza mpango wa Chakula kwa Elimu mkoani Mara ambao umeonesha mafanikio mbalimbali makubwa ikiwemo kupunguza utoro na kuboresha mahudhurio kwa asilimia 89 kutoka asilimia 84.5 mwaka 2017.

Amesema mpango huo unatekelezwa katika shule 231 na Kata 45 za Halmashauri ya Bunda mkoani Mara. Ameongeza kuwa mpango huo umeongeza uelewa wa wazazi katika kuchangia chakula shuleni.

Naye Kamishna wa Elimu, Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema pamoja na juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji, hakutakuwa na matokeo tarajali kama litasahaulika suala la upatikanaji wa chakula bora kwa wanafunzi wawapo shuleni.

Akiongea katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo, amesema Bunge linaunga mkono Mwongozo huo na kutoa wito kwa Wabunge na Madiwani kuendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika utoaji wa chakula shuleni.

Jumanne Webiro ambaye ni mzazi na Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya msingi Mariwanda 'B' ya mkoani Mara amesema wamekuwa wakitekeleza mpango wa Chakula kwa Elimu shuleni hapo kwa zaidi ya miaka 10 ambao umeleta matokeo mazuri sana ikiwemo kuongeza ari ya kukaa shuleni, utayari wa kujifunza, kuongeza ufaulu na kuondoa utoro. Amewaasa wazazi kuchangia huduma ya chakula na lishe shuleni ili kuboresha ufaulu wa watoto wao.

Read 601 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top