SERIKALI INAHAKIKISHA ELIMU TIBA INATOLEWA KATIKA VIWANGO VYA HALI YA JUU

Published on Sunday 04 December, 2022 07:52:07

Imeelezwa kuwa Serikali inatoa kipaumbele katika kuhakikisha elimu tiba inatolewa katika viwango ya hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.

Akizungumza katika Mahafali ya kumi na sita ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda (Mb) amesema katika katika kutekeleza azma hiyo na kuongeza fursa za masomo ya tiba,  Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kampasi ya MUHAS Mlongazila.

Amesema pia katika kuongeza hamasa na nafasi za masomo ya elimu tiba Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia  kupitia  mpango wa Samia Scholarship inatoa Ufadhili asilimia 100  kwa wanafunzi wanaosoma masomo hayo katika vyuo vya hapa nchini kuanzia mwaka huu wa masomo. 

Prof. Mkenda amewapongeza wanafunzi wote waliofaulu vizuri na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wanapokwenda katika jamii kwa kutoa huduma bora.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Dkt. Harrison Mwakyembe ameishukuru Serikali na Wizara kwa kukipatia Chuo hicho takribani bilioni 106.4 kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi za Mlongazila na Kigoma ambao utaongeza udahili wa wanafunzi katika fani za tiba.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Andrea Pembe amesema jumla ya wahitimu 1,389 wametunukiwa Shahada za Uzamivu, Uzamili, Shahada za kwanza na Stashahada mbalimbali za Chuo hicho.

Ameongeza kuwa katika mahafali hayo wahitimu 59 ni wa programu mpya 10 za Uzamili ambazo zimeanza kutoa wahitimu mwaka huu.

Prof. Pembe amezitaja programu hizo kuwa ni Magonjwa ya Damu na Saratani za Watoto, Uvumbuzi magonjwa ya fahamu kwa njia ya Mionzi,  Upasuaji wa Watoto, Magonjwa Mahututi, Mzunguko wa Damu katika upasuaji wa Moyo, Uuguzi katika fani ya magonjwa ya moyo, Uuguzi wa  Magonjwa ya Figo, Uuguzi wa magonjwa ya Figo,  Uugu?i wa magonjwa ya saratani,    Afya ya Jamii,  sayansi ya Utekelezaji na Uchumi na Sera za Afya.

Read 796 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top