SERIKALI IMEANDAA MWONGOZO WA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI WOTE WALISHINDWA KUREJEA VYUONI NJE YA NCHI

Published on Friday 17 December, 2021 17:13:11

Serikali imesema imeandaa Mwongozo wa Mafunzo Kwa Vitendo Kwa wanafunzi wote walioshindwa kurejea katika Vyuo wanavyosoma nje ya nchi kutokana na changamoto za Uviko 19 ili kuwawezesha kukamilisha masomo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (Mb)  leo Desemba 17, 2021 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji Tuzo ya Balozi wa China kwa walimu wanaofundisha Kichina na wanafunzi wanaosoma lugha hiyo nchini ambapo amesema mwongozo huo unahusisha wanafunzi wale ambao vyuo vyao vimeridhia utaratibu huo.

Amesema kuna baadhi ya vyuo haviko tayari kwa utaratibu huo wa wanafunzi kufanya mafunzo hayo na kutathminiwa na wakufunzi wa  hapa nchini, hivyo Serikali inaangalia utaratibu mzuri wa kuwawezesha kuhamishia masomo yao hapa nchini ili  kukamilisha mafunzo kwa kuwa hakuna tofauti ya masomo katika vyuo hivyo.

"Kwa kuwa hatujui ni lini janga hili la Uviko 19 litakwisha, bado tunaangalia njia nzuri ya kuwawezesha wanafunzi waliokuwa wakisoma nje ya nchi kukamilisha masomo yao hapa nchini kwa kuwa mafunzo waliokuwa wakiyachukua huko yanatolewa hata hapa nchini," amesema Profesa Ndalichako. 

Akizungumzia tuzo ya Balozi wa China kwa wanafunzi na walimu wanaosoma na kufundisha katika Kituo cha lugha ya Kifaransa, Waziri huyo amesema kuwa nchi hizi mbili zimekuwa na utaratibu wa kutoa ufadhili wa watu wake kujifunza lugha, ambapo amesema Serikali ya Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kila mwaka imekuwa ikitoa ufadhili kwa wanafunzi kumi kutoka China kuingia katika programu ya kujifunza Kiswahili.

Amewataka wanafunzi na walimu waliopata tuzo hiyo ambayo itawawezesha kupata ufadhili wa masomo katika vyuo vya nchini China kutumia fursa hiyo kusoma kwa bidii.

Balozi wa China nchini, Chen Mingjian amesema Serikali ya China imekuwa na utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Kitanzania ambapo kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 123 na walimu nane wamepatiwa ufadhili wa kulipiwa gharama zote za masomo katika vyuo vya nchini China.

Amesema China inatoa ufadhili huo kwa nia ya kuunga mkono jitihada za Serikali inazowekeza katika kuhakikisha watu wake wanapata elimu bora kwa ajili ya maendeleo ya nchi.

Naye Mwalimu wa Kichina katika Kituo cha kufundisha lugha ya Kichina kilichopo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Daud Masamilo ameishukuru Serikali ya China kwa kuwapatia nafasi ya ufadhili wa masomo na kuwashauri wanafunzi ambao wanapenda kusoma Kichina kuongeza bidii kwani lugha hiyo si ngumu kama wengi wanavyofikiria.

Read 562 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top