Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupandisha posho ya kujikimu ya wanafunzi wa elimu ya juu hadi kufikia Sh. Elfu kumi kwa siku.
Rais Samia amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na wawakilishi wa Jumuiya za Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania TAHLISO na ZAHLIFE katika viwanja vya Ikulu Chamwino jijini Dodoma.
Aidha amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuinua elimu ya juu kwa kuongeza fursa za upatikanaji wake ikiwemo kuongeza wigo wa mikopo na kuwataka kuhakikisha wanarejesha mikopo hiyo ili iwanufaishe na wengine.
“Labda niwaambie tumekamilisha mkataba na Benki ya NMB wa thamani ya Sh. Bilioni 200 ili wazazi ambao mishahara yao inapita benki waweze kukopa kwa ajili ya vijana wao," amesema Rais Samia.
Dkt. Samia amewataka wanafunzi kuwa na ufahamu kuhusu mwelekeo wa nchi na aina ya Taifa tunalotaka kulijenga ambalo litajitegemea kiuchumi huku akiwasisitiza kuweka mkazo katika masomo na kujiepusha na vitendo viovu.
Mhe. Samia ameupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu kwa namna unavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwa wakati.
"Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Katibu Mkuu na Timu yote ya Wizara kwa kazi nzuri sana mnayoifanya kuwahudumia watoto hawa na mipango mingi ambayo nimeiagiza Prof. Mkenda na timu yake wameibeba na kwenda kuitekeleza vizuri sana tena kwa muda mfupi. Zamani ilizoeleka unaagiza inakwenda kutekelezeka kwa muda mrefu ukiuliza unaambiwa fedha lakini sasa hivi ukiagiza linafanyika, tunasonga mbele," amesema Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amemshukuru Rais Samia kwa kutoa fursa ya kukutana na Wawakilishi hao na kumshukuru kwa kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu ambapo alipoingia madarakani ameongeza mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka TZS bilioni 464 hadi kufikia bilioni 654.
Mkenda ameongeza kuwa Wizara iliunda Kamati kwa lengo la kuangalia mfumo wa utoaji mikopo hususan kuangalia vigezo vitakavyoweza kutumika kuhahakisha mikopo inawafikia walengwa. Aidha amesema katika kuongeza wigo wa ugharamiaji elimu ya juu kupitia ufadhili wa Samia Scholarship wanafunzi 640 wanaosoma fani za Sayansi wamepata ufadhili katika Mwaka wa fedha 2022/23.
Katika hatua nyingine Mkenda amemuahidi Rais kuwa Wizara na Taasisi zinazosimamia Elimu ya kati na ya Juu zitaongeza ushirikishwaji wa serikali za wanafunzi kwa kuweka mfumo utakaorahisisha mawasiliano na viongozi hao.
“Mhe. Rais kwa kuanzia tumeteua mjumbe mmoja kupitia uongozi wa TAHLISO kuingia kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu (TCU). Tumeangalia kwa TCU sheria hairuhusu lakini wamesema wako tayari kuingiza mjumbe mmoja mwanafunzi katika baadhi ya vikao vyao ili kupitia huu ushirikishwaji changamoto ziweze kufikishwa na kutatuliwa kwa wakati," amesema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake rais wa TAHLISO, Frank Nkinda amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwenye Vyuo ya elimu ya juu kupitia Mradi wa HEET pamoja na kuondoa asilimia 6 ya tozo ya kutunza thamani ya fedha na asilimia 10 ya kuchelewa kurejesha mikopo.
Nkinda ameshukuru na kupongeza ushirikiano wanaopata kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTVET).