PROF. MKENDA: SIMAMIENI VIZURI MIRADI INAYOTEKELEZWA NA WIZARA

Published on Monday 11 April, 2022 12:52:24

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (Mb) amewataka watumishi wa Wizara ya Elimu kuhakikisha wanasimamia vizuri miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo ili ikamilike kwa wakati na kwa ubora.
 
Waziri Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 30 wa Baraza la Wafanyakazi ambapo amesema kukamilika kwa miradi hiyo ni kutoa fursa kwa watoto wa Kitanzania kupata elimu katika mazingira mazuri.
 
Prof. Mkenda amesema kazi kubwa iliyopo sasa ni kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora katika ngazi zote na kwamba mageuzi yanayofanyika kwenye elimu yakidhi matakwa na kujenga uwezo wa wanaohitimu kutoa huduma bora.
 
“Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 22, 2021 wakati akihutubia Bunge jambo kubwa alilosisitiza ni elimu na umuhimu wa kupitia mitaala yetu kuhakikisha elimu tunayoitoa inamuandaa mtu kulingana na mahitaji ya nchi na kimataifa kwa ajili ya utandawazi na kuweza kumudu kuendesha maisha,” amesema Waziri Mkenda.
 
Vilevile Waziri Mkenda amesisitiza  Mabaraza ya Vyuo Vikuu kuhakikisha wanasimamia kuhakiksha elimu inayotolewa inakuwa bora badala ya kuweka kipaumbele katika kuongeza nafasi za masomo.
 
“Elimu ni uwekezaji wa vizazi na vizazi, ukiwekeza kwenye elimu vizuri leo unawekeza kwa kizazi kimoja na kingine na uwekezaji mzuri kwenye elimu ni kuhakikisha ubora wa elimu wa sasa na vizazi vijavyo,” amesema Prof. Mkenda.
 
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Eliamani Sedoyeka ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema kufanyika kwa kikao hicho ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria katika sehemu za kazi juu ya ushirikishwaji ili kupata maoni ya watumishi katika utendaji kwa kuwa ni wao sehemu utekelezaji katika kutimiza malengo ya Wizara.
 
Aidha Prof. Sedoyeka amewataka watumishi kujitokeza kwa wingi katika zoezi la sensa ambalo linatarajia kufanyika kitaifa tarehe 23 Agosti, 2022. 
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania Taifa, Deus Seif amemueleza Waziri Mkenda kuwa  tija inayoonekana katika kazi inatokana na mshikamano na ushirikiano uliopo baina ya watendaji na kuahidi kuendeleza ushirikiano huo ili utendaji uendelee kuwa bora zaidi.
 
Kaulimbiu ya Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la mwaka huu ni “Sensa ya Watu na Makazi ni Msingi na Kichocheo cha Sera Bora na Mipango Endelevu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Tushiriki Kikamilifu.”
Read 215 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022