PROF. MKENDA AWATAKA WATANZANIA KUTUMIA LUGHA YA KISWAHILI KWA UFASAHA ILI KUENZI UTAMADUNI WETU

Published on Tuesday 05 July, 2022 05:32:29

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema watanzania lazima waenzi na kutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha.

Waziri Prof. Mkenda amesema hayo Julai 5, 2022 jijini Dar es Salaam  alipokuwa Mgeni Rasmi katika Mdahalo kuhusu Lugha ya Kiswahili na Elimu ambayo ni sehemu ya kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani Julai 7, 2022.

“Roho ya nchi ni utamaduni wake, sisi Watanzania ni lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha tunaongea Kiswahili fasaha, hili ni jukumu letu. BAKITA na BAKIZA muwe mstari wa mbele ili kukuza na kuendeleza matumizi ya Kiswahili na istilahi za Kiswahili” amesema Prof. Mkenda.

Katika kuhakikisha Kiswahili fasaha kinatumika, Prof. Mkenda amesema Wizara yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Barazala Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Braza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) katika kusukuma mbele masuala ya filamu ili kusaidia kukuza na kueneza Kiswahili ndani na nje ya nchi.

Waziri Prof. Mkenda ametumia fursa hiyo kuhimiza uandishi wa mashairi, riwaya, tamthilia pamoja na hadithi ili kusaidia kukuza lugha ya Kiswahili.

“Angalieni fursa za Kiswahili nje ya Tanzania, ukisoma Kiswahili, ni ‘dili’ na kitakupeleka ng’ambo, tunahitaji walimu wenye ufasaha katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza na uwezo mzuri wa kufundisha” amesema Prof. Mkenda.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani hapa nchini yatafanyika Julai 7, 2022 katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ambapo dunia nzima itasherehekea siku hiyo kwa mara ya kwanza baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutangaza rasmi Julai 7 ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.   
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni,Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema kuwa Serikali imeelekeza Balozi zote za Tanzania Ulimwenguni kuhakikisha zinaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani Julai 07, 2022.

“Tumeelekeza Balozi zetu kote Ulimwenguni kuhakikisha tarehe 07, 2022 wanaadhimisha Siku ya Kiswahili, siku hiyo tunataka Dunia itambue lugha hiyo kuwa Chimbuko lake ni Tanzania. Tunaamini Balozi hizo zitasaidia Kutangaza vyema lugha hiyo na kutoa fursa kwa watanzania katika kupata ajira ya kufundisha lugha hiyo Duniani" amesema Bw. Yakubu.


Ameongeza kuwa, Tanzania pia itashiriki katika maadhimisho hayo nchini Ufaransa ambayo ni Makao Makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ambapo itawakilishwa na baadhi ya Mawaziri pamoja na Msanii Mrisho Mpoto.

Read 220 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022