OLE NASHA: MSIWAGEUZE WATOTO WA KIKE MITAJI

Published on Friday 27 September, 2019 07:17:37

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka wazazi kuacha kuwageuza mitaji watoto wao wa kike kwa kuwaozesha mapema na badala yake wawasaidie katika kupata elimu ili baadaye wawe msaada  kwao na taifa kwa ujumla.

Ole Nasha ameyasema hayo leo alipofanya  ziara ya kikazi wilayani Itilima mkoani Simiyu ambapo amekagua  ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana katika shule ya sekondari Nkoma yenye uwezo wa kuchukua watoto 160 kwa wakati moja.

"Niwaambie kitu wazazi, kama unataka kumfanya mwanao wa kike mtaji basi mtaji mkubwa ni kumpa elimu na sio kumuozesha," alisema Ole Nasha.

Aidha Naibu Waziri Ole Nasha amewataka wazazi kuwekeza kwenye elimu ya watoto wao huku akisisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume, ambapo amesema katika jamii nyingi bado hawajawapa kipaumbele cha kupata elimu watoto wa kike.

“Kuna baadhi ya wazazi bado wanashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo. Nawaomba wazazi msishawishi watoto wa kike na kuwatilia vikwazo vya kukatisha masomo ili muwaozeshe. Mtoto wa kike ana nafasi ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.

Ole Nasha aliongeza kuwa serikali na wadau wa elimu wanatakiwa waendelee kutoa hamasa ya elimu kwa jamii, wanafunzi na wazazi ili miundombinu ya elimu inayojengwa iweze kutumika kwa faida ya wananchi wote katika kuboresha na kukuza elimu.

 Naibu Waziri Ole Nasha amepongeza  usimamizi wa fedha za miradi ya elimu katika wilaya hiyo kutokana na kutokuwepo kwa malalamiko yoyote ya matumizi mabaya ya fedha hizo.

Awali, akisoma taarifa ya ujenzi wa mabweni hayo, Mwalimu Mkuu wa shule ya sekondari Nkoma, Sara Matonya alisema mabweni hayo yamegharimu zaidi ya shilingi milioni 300 na kwamba kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa mabweni kumechochea hamasa ya wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia.

"Mabweni haya mawili yana uwezo wa kubeba wanafunzi 80 kila moja na yamesaidia wanafunzi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilometa 10 kufika shuleni. Wanafunzi wa kike pia wameepukana na vishawishi na mimba zilizokuwa zikiwasababishia kukatisha masomo," alisema Mwalimu Matonya.

Kwa upande wao wazazi na wanafunzi wameipongeza serikali kwa kutoa elimu bila malipo pamoja na kuwajengea mabweni, hali iliyopelekea kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi darasani, ufaulu na mwitikio wa elimu katika jamii.

“Tunaipongeza serikali kwa ujenzi wa mabweni haya ambayo yametupunguzia changamoto ya kutembea umbali mrefu na pia tumekuwa na muda mwingi wa kujifunza na kujisomea, na hivyo kutuwezesha kufanya vizuri katika masomo yetu,” alisema Myano Ngusa, mwanafunzi wa shule ya sekondari Nkoma.

Katika ziara hiyo Ole Nasha pia alikagua ofisi ya Uthibiti Ubora wilaya ya Itilima ambazo ujenzi wake umekamilika pamoja na majengo ya VETA yanayoendelea kujengwa katika kijiji cha Kanadi wilayani humo.

Read 1592 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top