Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu inayolenga kusaidia jamii na kukuza viwanda kupitia tafiti na bunifu zinazofanywa na wanafunzi wa Taasisi hiyo.
Hayo yamejidhihirisha kupitia Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kilimo Endelevu wa Taasisi hiyo Bi. Monica Nakei ambae anafanya utafiti wa mbolea asilia itokanayo na vimelea vya bakteria jamii ya rhizobia.
Akizungumza katika maonesho ya 28 ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yanayoendelea viwanja vya Themi Arusha Agosti 2, 2022 Mwanafunzi huyo amesema amefanya utafiti wa mbolea hiyo kupitia zao la soya na kwamba utafiti ukatapokamilika mbolea hiyo itakuwa tayari kwa matumizi.
Amesema katika utafiti wake amegundua kuwa mbolea hiyo ina faida nyingi ikiwemo kuongeza virutubisho vya nitrogeni na fosforasi kwa mimea ya Soya na kuimarisha afya ya udongo na kuweka usawa katika mfumo wa ikilojia ya udongo.
Bi. Monica ameeleza kuwa, faida nyingine ni pamoja na mazao yatokanayo na mbolea hiyo kutokuwa na kemikali zenye kuleta madhara kwa walaji na gharama yake ni nafuu kwa wakulima.
“Nawashauri wakulima wa soya (soyalishe) kutumia mbolea asilia ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwani mbolea hii pamoja na kuwa na thamani kwenye zao lenyewe inatunza mazingira kama maji, hewa na udongo,”amesema Mwanafunzi Monica.
Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela inashirikia maonesho ya 28 ya NaneNane yanayoendelea katika viwanja vya Themi jijini Arusha ambapo kupitia wanafunzi wake inaendelea kutoa elimu ya migomba iliyoboreshwa, kiatilifu biologia cha kudhibiti wadudu katika zao la Kabeji, upimaji wa udongo , chakula cha samaki chenye lishe, buheri wa Afya,Nutrano,NUSA,Omega -3DHA,Ngwara,Kweme na vyakula visivyo vya kemikali.