MRADI WA HEET KULETA MAGEUZI MAKUBWA ELIMU YA JUU

Published on Sunday 19 June, 2022 15:13:50

Benki ya Dunia yatoa takribani  trilioni moja kuwezesha
??Wakuu wa Vyuo watakiwa kusimamia Mradi vizuri

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo wa fedha takribani Shilingi trilioni moja ambazo zinakwenda kuleta mageuzi katika utoaji wa elimu juu. 

Akizungumza Jijiji Dar es Salaam wakati wa utiaji saini makubaliano ya utekelezaji Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na Vyuo Vikuu na Taasisi walionufaika amesema mkopo huo umelenga kuleta mageuzi ya kiuchumi kupitia utoaji wa elimu ya juu. 

Amesema Mradi huo unakwenda kujenga miundombinu, kununua vifaa wezeshi vya kujifunzia na kusomesha wahadhiri ambapo Vyuo Vikuu vya umma 14, Taasisi Tatu zilizo chini ya Wizara zinazosimamia elimu ya juu na Taasisi Tano zilizo chini ya Wizara ya Fedha watanufaika. 

Mradi wa HEET unakwenda kupeleka Vyuo Vikuu katika mikoa ambayo haina Vyuo hivyo kwa kujenga Kampasi zitakazokuwa zinalelewa na Vyuo Vikuu kamili ambavyo vinatekeleza Mradi huo. Kampasi hizo zitajengwa katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Lindi, Rukwa, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Manyara, Ruvuma, Kagera, Songwe, Katavi, Mara, Singida, pia Mradi utajenga Chuo Kikuu cha Taifa cha TEHAMA, Dodoma.


“Kwenye kujenga hizi Kampasi tutakachofanya ni kuendeleza maono ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan wakati anahutubia Bunge alisema kwamba mjaribu kutoa elimu bora ambayo inakidhi mahitaji kwa maana ya ujuzi na ufundi hivyo Kampasi zitakazojengwa tutaweka utaratibu kuwa hata kama watatoa Shahada ziwe ni za ujuzi,” amesema Waziri Mkenda. 

Waziri Mkenda amewataka wakuu wa Vyuo kuhakikisha wanasimamia vizuri matumizi ya fedha hizo ili malengo ya Mradi yaweze kutimia. Amesema mradi huo ukitekelezwa vizuri utawezesha upatikanaji wa miradi mingine itakayofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Awali Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe amesema Mradi huo unakwenda kuondoa changamoto kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini ambapo amesema ni vizuri waratibu wa miradi waliopo kwenye Taasisi wakawa na mawasiliano ya karibu na Wizara pale wanapopata changamoto ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati.

“Uzoefu unaonesha baadhi ya Taasisi zinachukua muda mrefu kutekeleza mradi, utiaji huu wa saini utasaidia kufuatilia kwa karibu na kuingilia kati kwa haraka endapo kutajitokeza changamoto zozote,” amesema Prof. Mdoe.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Nkainga Kaboko ameipongeza Wizara kwa kutimiza vigezo vya kupata mkopo huo na kwamba wako tayari kutoa ushauri pale wanapohitajika katika utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Vyuo, Mwenyekiti wa Makamu Wakuu wa Vyuo Vikuu vya Serikali, Prof. Evarist Liwa ameishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha na kuahidi kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili malengo yaweze kutimia.

Read 855 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022