MKENDA AONGOZA KIKAO KUJADILI MKAKATI KABAMBE UJENZI VETA 63 ZA WILAYA

Published on Wednesday 30 November, 2022 08:25:05

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema mageuzi ya elimu yanayokuja yanakwenda sambamba na kuandaa mazingira ya kuhakikisha elimu ujuzi inapatikana.

Mhe. Mkenda ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha pamoja cha  Menejimenti ya Wizara na ile ya VETA chenye lengo la kujadili kwa pamoja mikakati ya utekelezaji wa ujenzi wa VETA 63 za wilaya na moja ya mkoa.

Amesema moja ya eneo linaloangaliwa katika kutoa elimu ujuzi ni kupitia vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) hivyo ni   vizuri kuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha VETA 63 za Wilaya na moja ya mkoa ujenzi unaanza.

 "Nataka twende pamoja, katika kuweka historia hii; tunakwenda kufanya mageuzi makubwa ya elimu kwa kuhakikisha  tunatoa elimu ujuzi, sasa kazi ya mapitio ya Sera  na Mitaala inakwenda vizuri na tuko tayari kufanya wasilisho kwa ajili ya mjadala wa Kitaifa, sasa nataka huku kwenye ujenzi wa VETA 63 ambako elimu ujuzi inapatikana kuende kwa kasi na kwa  wakati ,"amesema Prof. Mkenda

Amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Wizara imetenga fedha Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa VETA hizo hivyo  kutaka   mkakati wa kuhakikisha ujenzi unaanza mapema na kujengwa kwa usahihi kwa kuzingatia taratibu zote husika.

Akizungumzia ujenzi wa Kampasi za Vyuo Vikuu katika mikoa 14 kupitia Mradi wa HEET Mhe. Mkenda amewataka Wakandarasi waliopo wizarani kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji na kushirikiana na  na Vyuo Vikuu kujua mikakati iliyowekwa na Vyuo mama kuhusu ujenzi huo ili kazi iweze kwenda kwa haraka.

Akizungumzia maandalizi ya ujenzi wa VETA hizo Mhandisi George Sambali kutoka VETA  amesema mpaka sasa kati ya wilaya 63 zinazojengewa VETA wilaya 59 tayari zina maeneo.

Read 250 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top