Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Carolyne Nombo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa umahiri, weledi na ubunifu ili malengo ya sekta ya elimu, Sayansi na Teknolojia yaweze kufikiwa.
Prof. Nombo ametoa wito huo jijini Dodoma wakati wa mapokezi yake na Naibu Katibu Mkuu Dkt Franklin Rwezimula baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amesema Wizara hiyo imepewa majukumu makubwa ya kuhakikisha elimu inayotolewa kwa watanznia inakuwa bora na kuimarisha Sekta ya Sayansi na Teknolojia.
Ameongeza hivi sasa wizara ipo katika hatua za mwisho za kuhuisha sera ya elimu na mafunzo ta 2014 na Mitaala,huku akisisitiza kuwa si Tanzania pekee inayofanya mageuzi hayo bali Dunia nzima ipo katika kufanya mageuzi ya elimu.
"Mageuzi katika utendaji wa kufanya kazi kwa weledi, umahiri , ubunifu na kwa uwazi ni muhimu ili kufikia yale mageuzi tunayoyatamani katika sekta ya elimu", amesisitiza Katibu Mkuu.
Prof. Nombo amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaamini na kumpa nafasi katika utumishi huo.
Aidha amewashukuru Makatibu Wakuu waliotangulia kwa kuweka misingi imara katika kuelekea mageuzi nchini.
Naye Naibu Katibu Dkt. Franklin Rwezimula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuani na kumpa nafasi ya kutumikia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, huku akiahidi ushirikiano kutoka kwa watumishi ili kuendelea kuboresha sekta ya elimu.