Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema elimu bora itapatikana na kuhakisi mahitaji ya nchi endapo kama Maafisa Uthibiti Ubora watakuwa wanaharakati wa mabadiliko katika maeneo yao ya kazi.
Pamoja na hilo,amewataka kuhakikisha malezi ya wanafunzi yanapewa kipaumbele ili kutengeneza kizazi bora kwa sasa na baadaye.
Waziri Mkenda amesema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha Viongozi na Maafisa wa Uthibiti ubora wa Shule makao makuu na Wathibiti Ubora wa shule Kanda na Wilaya Tanzania Bara.
Amesema Wathibiti ubora wana nafasi kubwa katika kusimamia ubora wa elimu inayotolewa na kuwataka kuendelea kujiongeza katika utendaji kwani wao ndio mboni ya jicho la elimu nchini.
"Na ndio maana nimefurahi sana niliposikia nakuja kuzungumza nanyi ili kueleza umuhimu wenu. Ninyi ni mboni wa elimu hapa nchini, manatakiwa kupambana mambo yakiwa hayaendi vizuri, tizameni kinachoendelea huko katka maeneo yenu ya kazi Serikali imeboresha mazingira ya utendaji wenu jitoeni tuendelee kujituma,"amesema Prof. Mkenda
Amesema kutokana na Utandawazi na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ni vizuri kujua namna ya kuendana nayo ili watoto wawe na malezi mazuri.
"Malezi ni pamoja na kujali afya za watoto, tushiriki kuhakikisha tunasimamia ujenzi wa vyoo katika maeneo yetu, halmashauri zitenge fedha kujenga vyoo ili changamoto hiyo iweze kuisha", ameongeza Prof. Mkenda
"Nimeongea na Waziri mwenzangu Mhe. Dorothy Gwajima tupitie miongozo yote watoto wanaaza shule wakiwa wadogo hapa suala la malezi ya mtoto katika maadili ni muhimu," ameongeza Prof. Mkenda
Kwa upande wake Naibu katibu Prof. James Mdoe amesema Wizara ya Elimu kwa sasa inaendelea na mapitio yaSera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 hivyo amesema wathibiti ubora ni wadau muhimu katika hilo hivyo ni muhimu wakashiriki katika kutoa maoni ya kuboresha sera kwa kuwa wanathibiti ubora wa elimu nchini.
Nae Kamishna wa Elimu Tanzania Dkt. Lyabwene Mtahabwa amesema kiongozi bora ni yule ambae nafanya watu wengi kumfuata badala ya kumkimbia huku akisiliza na kuwaasa wathibiti ubora hao kuwa wasikilizaji wazuri wa walimu na ndio maana kuna muhamo wa ruwaza.
Dkt Mtahabwa amewaasa pia katika kutoa mrejesho wa yale waliyobaini kwenye kazi zao kuangalia lugha nzuri ya mawasiliano kwa walimu.
"Kwa kiasi kikubwa kufeli kwa Taasisi yoyote kunategemea mkuu wa taasisi hivyo mnatakiwa kuwa viongozi wazuri katika kusimamia kazi katika maeneo yenu,"ameongeza Dkt. Mtahabwa
Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Idara ya Uthibiti ubora wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bibi Euphrasia Buchumu amesema idara hiyo ina jukumu kubwa ambalo kuangalia viwango vya utoaji elimu nchini.
Ametaja baadhi ya mafanikio ya idara hiyo kuwa ni kubadili mfumo wa uthibiti ubora kutoka kuwa ukaguzi kuwa uthibiti, ujenzi wa Ofisi 55 zimejengwa ambazo zimeongeza ari ya utendaji kazi.
Aidha Mkurugenzi Buchuma amemweleza Waziri Mkenda kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 idara pamoja na mambo mengine inatarajia kuweka Mfumo wa kielektoniki ili kutoa taarifa vizuri, Kuimarisha ikama na Kujengea uwezo wathibiti ubora wa shule.
Akizungumza kwa niaba ya Wathibiti Ubora wa Shule Bibi Bibi Edith Mwijage Mthibiti Mkuu Ubora wa Shule Kanda ya Magharibi amemuhakikishia Waziri Mkenda kuwa watahakikisha wanatekeleza yale yote aliyowaambia ili elimu iendelee kuwa bora.