Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt.Francis Michael amewataka watumishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kufanya kazi kwa weledi, nidhamu katika kuhakikisha suala la elimu linaendelea kuimarika nchini.
Dkt.Michael ameyasema hayo leo tarehe 11/7/2022 jijini Dar es salaam alipofanya ziara katika Taasisi hiyo ambapo amesema Serikali inawategemea katika kusaidia utoaji wa elimu nchini.
"Nawaomba mfanye kazi kwa weledi na kuhakikisha suala la elimu na haswa haya maboresho ya mitaala yanayoendelea yafanyike vizuri,"amesema Dkt.Michael.
Aidha Dkt.Michael amemshukuru Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna anavyoendelea kuwajali watumishi wa umma kwa kujali maslahi yao na kuwataka watumishi wa TET kutomwangusha Rais, na badala yake wafanye kazi ipasavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba amesema kuwa wameshukuru ujio wa Katibu Mkuu na kuwa TET inaendelea kufanya kazi zake katika kuzingatia misingi ya kiutumishi na kuwa suala la maboresho ya mitaala linaloendelea litafanyika vizuri.
Katibu Mkuu katika ziara yake aliambatana na Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Moshi Kabengwe.