BILIONI 64.9 ZA UVIKO 19 KUTUMIKA KUIMARISHA ELIMU MAALUM, UFUNDI NA UALIMU

Published on Tuesday 26 October, 2021 07:58:10

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema itatumia fedha kiasi cha Sh. bilioni 64.9 zilizotokana na Mpango wa  Maendeleo  kwa  Ustawi wa Mapambano dhidi ya UVIKO 19 kwa ajili ya kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na kuimarisha mazingira ya utoaji wa Elimu ya ualimu.

Kauli hiyo imetolewa 23 Oktoba, 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako Jijini Dodoma alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu matumizi ya fedha hizo.

Akitolea ufafanuzi matumizi ya fedha hizo amesema Shilingi 1,477,000,000.00 zilizotengwa kwa ajili ya kuimarisha ujifunzaji na ufundishaji kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum zitatumika kuchapa vitabu kwa ajili ya wanafunzi 353 wasioona na 3,591 wenye uoni hafifu wa elimu ya sekondari pamoja na kununua vifaa saidizi kwa wanafunzi 410 walioko katika Vyuo Vikuu 11 vya Serikali.

Kwa upande wa kuimarisha Elimu ya ufundi, Shilingi 57,985,000,000.00 zimetengwa ambapo zitatumika kukamilisha ujenzi na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo 25 vya Ufundi Stadi vya Wilaya, kukamilisha ujenzi na kuweka samani katika Vyuo vya VETA vinne ngazi ya Mkoa katika mikoa ya Njombe, Rukwa, Simiyu na Geita, kujenga mabweni katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Morogoro, kuimarisha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kwa kununua vifaa na mitambo ya kufundishia na kujifunzia na kukamilisha jengo la Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) litakalokuwa na kumbi za mihadhara, vyumba vya madarasa, maabara na ofisi.

Akizungumzia uimarishaji wa mazingira ya utoaji wa elimu ya Ualimu ambayo imetengewa Sh.  5,440,000,000.00, Waziri Ndalichako amesema vyumba vya madarasa 41, kumbi 3 za mihadhara na mabweni 15 yatajengwa kwenye baadhi ya vyuo vya ualimu na kuwekewa samani.

Aidha, Waziri Ndalichako amewataka watendaji wa Wizara na Taasisi zinazotekeleza miradi hiyo kuhakikisha inakamilika kabla au ifikapo Mei 30, 2022 na kununua vifaa kulingana na bei ya soko, ikiwa ni pamoja na kutotumia fedha  hizo kulipana posho.

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu kuandaa mfumo wa uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa mradi utakaowezesha kubaini changamoto zitakazojitokeza wakati wa utekelezaji na kuchukua hatua stahiki.

Read 429 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top