Bilioni 100 Kuimarisha elimu ya Ufundi

Published on Tuesday 09 August, 2022 11:12:00

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejizatiti katika kutoa elimu ujuzi na hivyo itaendelea kuwekeza katika elimu ya ufundi ikiwemo ujenzi wa Vyuo vya VETA  katika kila wilaya na Mikoa.

Amesema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Chuo cha VETA cha Wilaya ya Mbarali kinachojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia chini ya Mradi wa Kukuza Ujuzi (ESPJ).

Ametumia nafasi hiyo kuwataka wanachi wa Mkoa wa Mbeya na hususan Wilaya ya Mbarali kuhakikisha wanakitumia chuo hicho kupata ujuzi kulingana na shughuli zao za kiuchumi.

"Najua hapa kuna vijana wengi mna shughuli mbalimbali tumieni sana chuo hiki kupata ujuzi na kuongeza tija katika kazi zenu na hata kuanzisha viwanda  vya uchomeleaji na vingine," amesema Mhe. Samia

Akimkaribisha Rais Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema ujenzi wa chuo hicho umefikia asilimia 95 na kwamba hadi kukamilika utatumia Shilingi Bilioni 2.7.

Ameongeza kuwa  Chuo hicho kinatarajiwa kukamilika mwezi Septemba  mwaka huu na kuanza kudahili wanafunzi wa kozi fupi wapatao  240 na mwezi Januari 2023 kudahili wanafunzi wa kozi za muda mrefu wapatao 500.

Mhe. Mkenda amemshukuru Rais kwa kuongeza uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa VETA kupitia bajeti ambapo Bilioni 100 zimetengwa kwa ajili hiyo.

Chuo cha VETA Mbarali ni sehemu ya Vyuo 25 vya Wilaya  na vinne vya Mikoa vinavyojengwa kupitia mradi huo ambao  unaogharimu takriban Biknk 49. Aidha amempongeza Rais kwa kutoa fedha za Mpango wa Mapambano dhini ya Uviko na Ustawi ambazo pia zime changia katika kukamilisha vyuo hivyo.

Mkenda ameeleza kuwa Wizara kwa sasa inafanya tathmini ya kujua uwezo wa wanafunzi wanaotoka VETA  katika kazi na uwezo wa kuajiriwa kwao kupitia waajiri mbalimbali. Lengo ni kuhakikisha elimu inayotolewa ni bora na sahihi kulingana na uhitaji wa soko pamoja na kuongeza kasi ya kuandaa Walimu wa Ufundi.

"Mhe Rais katika fedha za Uviko tumewekeza katika Chuo cha Walimu wa Ufundi Morogoro na pale Chuo cha Ufundi Arusha. Lengo letu ni pamoja na kasi ya kuongeza Vyuo wawepo walimu wa ufundi wa kutosha" amesema Mhe. Mkenda

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa VETA amesema Vyuo  vyote vya VETA vya Wilaya vinatoa kipaumbele katika mafunzo yanayoendana na shughuli za kiuchumi na Mkoa na Wilaya husika huku akitolea mfano Chuo cha Mbarali ambacho kitatoa mafunzo ikiwemo uchomeaji, ufundi mitambo, kompyuta, ukatibu muhtasi, ushonaji na umeme wa majumbani.

Read 504 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022