Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi Victoria Kwakwa Julai 11, 2022 ametembelea shule ya Sekondari Turiani Jijini Dar es Salaam ili kujionea maendeleo ya Programu ya SEQUIP ambayo sehemu ya utekelezaji wake ni mpango wa kuwarudisha shuleni watoto walioacha masomo kutokana na sababu mbalimbali ili waweze kuendelea na masomo yao.
Akizungumza shuleni hapo akiwa ameongozana na mwenyeji wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof Adolf Mkenda kiongozi huyo amesema amefurahi kupata nafasi ya kutembelea shule hiyo na kuona mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendeleza sekta ya elimu ili kuzalisha nguvu kazi.
Amepongeza kwa hatua aliyochukuliwa na Mhe. Rais ya kuwapa tena fursa wanafunzi ambao walikatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ili wapate elimu ambayo itawawezesha kujiletea maendeleo kwao wenyewe na familia zao pamoja na kuchangia katika uchumi wa Taifa.
Kwakwa amesema Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu bora kwenye miundombinu na mazingira salama ya kujifunzia pamoja na kuondoa changamoto zinazokwamisha mchakato wa ujifunzaji.
Akizungumza katika ziara hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof Adolf Mkenda amesema Serikali ina mkakati mkubwa wa kuhakikisha watoto wote walioacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito wanarudi na kuendelea na masomo yao.
Kiongozi huyo amesema benki hiyo imefadhili programu ya SEQUIP ambayo imewezesha kuwarudisha shuleni wanafunzi wapatao 3,333 ambao waliacha shule kutokana na sababu mbalimbali ambapo takribani wanafunzi 900 wamerudi katika mfumo rasmi na wengine katika mfumo wa elimu mbadala.
Ameongeza kuwa Makamu wa Rais huyo amefika katika shule hiyo ili kuona na kuongea na mabinti waliorudi shule kupitia programu ya SEQUIP inayofadhiliwa wa Benki ya Dunia ili kuangalia maendeleo yao.