WAZIRI NDALICHAKO: WATENDAJI TEKELEZENI MRADI WA HEET KWA WAKATI NA UBORA

Published on Saturday 09 October, 2021 12:10:59

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (Mb) amewataka watendaji  wanaohusika na utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kutekeleza  mradi huo kwa wakati na kwa ubora.

Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam Septemba 9, 2021  katika Kikao kazi kati ya Uongozi wa Wizara na Watendaji hao ambapo amesema mafanikio ya Mradi huo pamoja na kuimarisha Elimu ya juu nchini pia itakuwa ni moja ya chachu za kuwezesha kupata fedha zaidi kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha elimu nchini

"Tarehe 27 Septemba mwaka huu nilipata fursa ya kuongea na Makamu Rais wa Benki ya Dunia kuhusu fedha za mradi mpya unaolenga kuboresha elimu msingi  ambao awali ulipata Dola milioni 200, lakini nilimuomba watuongezee ifike USD milioni 500 waliridhia na alipodadisi zaidi  kuhusu uwezo wa kutumia fedha hizo  nilimwambia atupime kupitia utekelezaji wa mradi wa HEET, hivyo naamini tukitekeleza vizuri mradi huu utatuwezesha kupata fedha zaidi na ndio lengo la kukutana leo tuweke mikakati na kukubaliana kutekeleza mradi wa HEET kwa mafanikio, " amefafanua Prof. Ndalichako.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga (Mb) akiongea katika kikao kazi hicho amesema mradi wowote ili ufanikiwe unatakiwa kuwa na rasilimali ambazo ni vifaa, rasilimaliwatu, fedha, uongozi na muda ambapo ameelekeza uongozi kusimamia vizuri rasilimali hizo ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa mradi.

"Ni suala la Menejimenti kuhakikisha kuwa vitu hivi vyote vinakuwepo na kunakuwa na timu itakayosimamia rasilimali hizi kuhakikisha zinatumika kikamilifu kufanikisha utekelezaji wa mradi," amesema Mhe. Kipanga.

Mradi wa HEET wenye thamani ya Shilingi bilioni 985.5 unalenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika Vyuo Vikuu 14 vya Serikali na Taasisi tatu zilizo chini ya Wizara ambazo ni TCU, HESLB na COSTECH kwa kuboresha miundo mbinu, kusomesha Wahadhiri zaidi ya 600, kuhuisha na kuanzisha Mitaala zaidi ya 290 na kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 40,000 hadi 100,600 ifikapo 2026.

Read 1084 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022