WANAFUNZI MWAKA WA KWANZA WALIOPATA MIKOPO WAFIKIA 46,838

Published on Monday 04 November, 2019 10:54:51

Jumapili, Novemba 3, 2019

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya tatu yenye jumla ya wanafunzi wa mwaka kwanza 4,785 waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 14.3 bilioni na hivyo kufanya jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopata mikopo yenye thamani ya TZS 162.86 bilioni hadi sasa kufikia 46,838.

Orodha ya kwanza ilitolewa Oktoba 17 mwaka huu na ilikuwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 30,675 waliopata mikopo yennye thamani ya TZS 113.5 bilioni. Orodha ya pili ilitolewa Oktoba 26 mwaka huu ikiwa na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 11,378 waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 35.06 bilioni.

Taarifa iliyotolewa leo (Jumapili, Novemba 3, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru imeeleza kuwa wanafunzi waliopata mikopo katika awamu ya tatu wanaweza kupata taarifa zao kupitia akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account.

Pamoja na SIPA, Badru amesema majina yote ya waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo katika awamu hii ya pili yanapatikana katika mtandao wa HESLB wa uombaji mkopo (https://olas.heslb.go.tz) na tovuti ya Bodi (www.heslb.go.tz).

“Awamu hii ya tatu inajumuisha wanafunzi wahitaji ambao wamekamilisha taratibu za udahili pamoja na kukamilisha marekebisho ya maombi yao yaliyokuwa na dosari … tutaendelea kufanyia kazi maombi yanayorekebishwa na wale wenye sifa watapangiwa,” amesema Badru.

Kuhusu taratibu za malipo kwa wanafunzi, Badru amesema fedha za wanafunzi waliopata mikopo zimeshapelekwa vyuoni na vyuo vimeleekezwa kuhakikisha fedha zinawafikia wanafunzi walengwa mara wanapofika na kukamilisha taratibu za usajili.

“Serikali imeshatupatia TZS 125 bilioni ambazo tulikuwa tunazihitaji kwa ajili ya malipo ya robo ya kwanza ya Oktoba hadi Disemba mwaka huu na sisi tumeshatuma vyuoni na maafisa wetu wameanza kwenda vyuoni ili kukutana na wanafunzi na kutatua changamoto iwapo zitajitokeza,” amesema Badru.

Badru amesema katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imetenga TZS 450 bilioni kwa ajili ya jumla ya wanafunzi 128,285. Kati yao, wanafunzi 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo ya mwaka wa pili, tatu na kuendelea.

Bodi inapenda kuwasihi waombaji wa mikopo kuwa watulivu wakati mchakato wa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wenye sifa kwa awamu inayofuata ukiendelea.

Mwisho.

Read 3718 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 296 3533
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Tanzania Census 2022