UJENZI KAMPASI YA KIKULETWA WAENDA KASI

Published on Saturday 04 March, 2023 11:21:18

Chuo cha Ufundi Arusha Kimepongezwa kwa hatua nzuri ya ujenzi wa Kampasi ya Kikuletwa iliyopo Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro inayojengwa kupitia Mradi wa Kujenga Ujuzi kwa Maendeleo na Uingiliano wa Kikanda katika Afrika Mashariki (EASTRIP)  unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Pongezi hizo zimetolewa leo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omari Kipanga (Mb) alipotembelea na kukagua ujenzi unaoendelea kwenye kampasi hiyo. Mheshimiwa Kipanga ameoneshwa kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na kuahidi serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kumaliza ujenzi huo kwa wakati.
“Leo tumefika eneo hili, tumezunguka maeneo yote, mradi unaendelea vizuri, tuna wakandarasi wawili ambao wanajenga eneo hili, mradi upo kwenye hatua nzuri tuwashukuru sana wakandarasi na wasimamizi wa mradi huu na sisi kama Wizara na Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha lile fungu la fedha ambalo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameshalitoa, zaidi ya bilioni 200 zitakapokuwa zinahitajika zije kwa wakati” alisema Mhe. Kipanga.
Aidha Mhe. Kipanga ametoa wito kwa wasimamizi wa mradi kusimamia mradi kwa ukaribu na kuhakikisha kwamba kazi inafanyika usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea wakati wa kuchimba msingi.

“Natoa wito kwa wajenzi kwa yale maeneo ambayo tuko nyuma kidogo kufanya kazi usiku na mchana ili kufidia muda uliopotea ili ifikapo mwezi wa tisa majenzo haya yaweze kuwa tayari na serikali kukabidhiwa tayari kwa vijana wetu kupata ujuzi hapa.
Naye mshauri wa ujenzi wa mradi huo Mhandisi Mringo Yasin ameeleza kwamba wamejipanga kuhakikisha vifaa vyote vya ujenzi vinafika eneo la ujenzi kwa wakati.
“Tunategemea kumaliza huu mradi kwa muda unaotakiwa, tunachosisitiza kwa wakandarasi ni kuhakikisha kuwa masika inayokuja wawe wameleta vifaa vya kutosha ili changamoto ya barabara itakayotokea tuwe tunaweza kuendelea na kazi” alieleza Mhandisi Yasin.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Masama- Rundugai Bw. Simbano Waziri ameishukuru serikali kwa kuleta mradi huo kwenye Kata yake ambao una manufaa mengi kwa jamii inayozunguka ambapo mpaka sasa vijana Zaidi ya asilimia sabini walioajiriwa kufanya kazi za ujenzi wanatoka kwenye kata hiyo na kuna vijana wengi kwenye Kata hiyo ambao wanasoma kwenye Kampasi ya Kikuletwa.
Chuo Cha Ufundi Arusha kimepata jumla ya shilingi bilioni 37 za kitanzania kutoka Benki ya Dunia kupitia Mradi wa EASTRIP wenye lengo la kuboresha Kampasi ya Kikuletwa kuwa kituo cha Umahiri kwenye Nishati Jadidifu.

Read 418 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top
Kituo cha Huduma kwa Mteja