TANZANIA NA AFRIKA KUSINI ZASAINI HATI YA MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO KATIKA MAMBO MBALIMBALI YA ELIMU YA MSINGI IKIWEMO KUFUNDISHA KISWAHILI

Published on Thursday 07 July, 2022 11:19:27

Serikali imesema itaongeza nguvu kazi, miundombinu na bajeti kwa taasisi na vyuo vinavyofundisha kiswahili ili viendelee kuandaa wataalam zaidi watakaotumika Duniani kote.

Akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yanayofanyika jijimi Dar es Salaam kwa njia ya simu Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema Serikali itaendelea kutoa nyenzo na mafunzo ya kisasa kwa wakalimani, waandishi wa vitabu, wafundishaji wa Kiswahili kwa wageni.

Katika Maadhimisho hayo, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Elimu ya Msingi ya Jamhuri ya Afrika Kusini zimetia saini Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika mambo mbalimbali ya Elimu ya Msingi ikiwemo kufundisha kiswahili.

Utiwaji wa saini umefanywa mbele ya  Mhe. Philip Isidor Mpango  Makamu wa Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda kwa upande Tanzania na kwa Jamhuri ya Afrika Kusini umefanywa na Waziri wa Elimu ya Msingi Matsie Angelina Motshekga 

Akiongea kabla ya utiaji wa saini Prof. Mkenda amesema baada ya kukamilika kwa maandalizi ya Hati hiyo Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza kutiwa saini rasmi makubaliano hayo siku ya Kiswahili Duniani.

"Kazi ya kuandaa makubaliano haya ilifanyika kwa muda ikiongozwa na viongozi mbalimbali ambapo baada ya kukamilika Rais alituagiza tusaini makubaliano haya leo katika siku hii  muhimu  kwa nchi yetu," amesema Pro. Mkenda

Naye Matsie Angelina Motshekga, Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini amesema lengo la kusaini hati hiyo ni kufundisha Kiswahili katika shule za msingi na vyuo pamoja na kukisambaza nchi nzima ili kuwawezesha waafrika Kusini waweze kuitumia lugha ya Kiswahili.

Motshekga ameongeza kuwa kwa Afrika Kusini Kiswahili ni zaidi ya lugha kwani ni muhimu sana kwani kitasaidia kuunganisha watu wake na Bara la Afrika ambapo Kiswahili kinaongelewa zaidi.

" Kiswahili kwa Afrika Kusini kitaunganisha watu wa Tanzania na kwetu pamoja  na kuimarisha mahusiano ya muda mrefu yaliyopo kati ya nchi hizi mbili, na ni lazima tuhakikishe lugha hii inaunganisha watu wetu hususani vijana" ameeleza Waziri huyo wa Afrika Kusini .

Read 868 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top