SHULE MPYA YA SEKONDARI YA MFANO KUJENGWA DODOMA

Published on Saturday 10 April, 2021 14:38:42

Serikali inajenga shule mpya ya sekondari ya mfano Iyumbu Jijini Dodoma itakayokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000 kwa wakati mmoja.

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema shule hiyo itakayokuwa na mchepuo wa Sayansi itakuwa na miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia na mazingira bora ya kusomea ikiwemo viwanja vya michezo na nyumba za walimu.

Ameongeza kuwa mpaka kukamilika kwake ujenzi wa shule hiyo utagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 17.

Prof. Ndalichako amesema pamoja na kuwa shule ya mfano, itachukua wanafunzi wenye ufaulu wa kawaida ili waweze kusoma kwenye mazingira yenye mahitaji yote ikiwemo miundombinu ya kisasa, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na walimu wa kutosha ili kuwawezesha kufanya vizuri katika masomo yao.

"Wakati Mhe Rais anawaapisha Makatibu Wakuu, kwenye sekta ya Elimu alisisitiza kuendelea kukamilisha na kujenga miundombinu ya Elimu kwa hiyo hii ni moja ya kazi zinazoendelea," amesema Prof. Ndalichako.

Aidha, Waziri Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt. Leonard Akwilapo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa wakati na ubora

Ndalichako amewasihi SUMA JKT kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wanamaliza ujenzi ifikapo Januari 2022.

Katika ziara hiyo Waziri Ndalichako aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Omary Kipanga na Naibu Katibu Mkuu, Prof. Carolyne Nombo.

Meja Philemon Komanya ambaye ni Msimazi wa Mradi huo amesema ujenzi wa Mradi umefikia asilimia 28 na ameahidi kuwa watahakikisha wanafikia lengo walilokubaliana la kukamilisha ifikapo Januari, 2022.

Read 4934 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top