Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uingereza inatarajia kutekeleza Mradi wa Shule Bora wenye lengo la kuboresha mazingira ya shule na kutoa mafunzo kwa walimu.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afrika katika Serikali ya Uingereza, James Duddridge ambao pia wametembelea shule ya Sekondari Kibasila.
Waziri Ndalichako ameongeza kuwa Serikali ya Uingereza ni moja kati ya wadau muhimu katika sekta ya elimu ambapo pamoja na mambo mengine imewezesha utekelezaji wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) na Mradi wa Kuboresha Elimu (Equip T) ambao umetekelezwa katika Mikoa tisa.