BAJETI YA UTAFITI NCHINI KUONGEZWA

Published on Monday 24 May, 2021 22:48:31

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa ameiagiza Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kuongeza Bajeti ya Utafiti kuanzia mwaka wa Fedha 2021/22.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyofanyika Chuoni hapo, ambapo amesisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha utafiti na kuendeleza ubunifu Nchini ili uweze kubiasharishwa, kutumika katika Viwanda na hatimae kuchangia Uchumi wa Nchi. 

"Nimeona ubunifu na tafiti zinazofanywa na vijana wetu kuanzia wiki mbili zilizopita pale Dodoma MAKISATU, Serikali  inaahidi kuwekeza zaidi katika kuwaendeleza, hivyo naagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na kuwa Bajeti yenu imepita mfanye mapitio na kuongeza Bajeti katika eneo hilo ili tafiti hizi na ubunifu uwe na tija kwa Taifa letu," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa kupitia Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22  Wizara imepanga kuimarisha Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na kwamba utafiti na ubunifu vitaendelea kutiliwa mkazo ili kuhakikisha kuwa Taifa letu linanufaika na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji mali na utoaji huduma kwa jamii.

Ameongezea kuwa mkazo pia umewekwa katika kuhakikisha Vituo Atamizi zaidi vinaanzishwa  ili kulea na kuendeleza Ubunifu na Tafiti nchini. 

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amemshukuru Waziri Mkuu kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi na kufika kujionea umahiri wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam . 

Ameongeza kuwa mwaka huu zaidi ya watafiti na wabunifu 218 wakiwemo wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo hicho wameingia katika kushindanishwa baada ya mchujo katika vitengo na idara mbalimbali za Chuoni hapo.

Pia ameongeza kuwa hii ni mara ya Sita kwa Wiki ya Utafiti na Ubunifu kufanyika na kwamba mwaka huu itahusisha mijadala  na kongamano litakaloshirikisha wenye viwanda, waajiri pamoja na watafiti.

Read 1582 times

Contact

  • Name:    Permanent Secretary
  • Address: Government City
  • Mtumba Area - Afya Street
  •               P.O.Box 10
  •               40479 Dodoma
  • Tel:        +255 26 216 0270               
  •                +255 737 962 965
  • Email:    info@moe.go.tz
  • Zonal SQA Offices Contacts
Top